Sababu wakala wa ndege za Serikali kuhamishiwa ofisi ya Rais hii hapa

Tuesday April 16 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika akitoa ufafanuzi kwanini Serikali haijapandisha mishahara ya watumishi, wakati bunge lilipokuwa likipitisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Si unakumbuka ile hoja ya Zitto Kabwe kutaka kujua sababu ya Wakala wa Ndege za Serikali kuhamishiwa Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, basi jana jioni Jumatano Aprili 15, 2019 Serikali imetoa majibu ya jambo hilo.

Katika hoja yake aliyoitoa katika mjadala wa bajeti ya ofisi hiyo mwaka 2019/2020, Zitto ambaye ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini alihoji wakala huo kuhamishwa, akitilia shaka kuwa huenda kuna jambo linafichwa.

 

Akichangia mjadala wa bajeti hiyo Ijumaa iliyopita, Zitto amesema: “Nimesoma hotuba ya ofisi ya Rais ukurasa wa 87,  Bunge linajulishwa kuwa kwa mujibu wa GN (Gazeti la Serikali) 252 ya 2018 kwa sasa wakala wa ndege za Serikali umehamishiwa ofisi ya Rais kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

“Mwaka 2017/18 tulitenga Sh509 bilioni, mwaka unaofuata Sh497 bilioni na mwaka huu zinatengwa Sh500 bilioni kwa ajili ya ununuzi ya ndege za ATCL (Shirika la Ndege Tanzania) lakini tunajua ATCL hawamiliki ndege wanakodisha zinamilikiwa na wakala wa ndege za Serikali.

“Halafu tunapitisha huku lakini tunategemea CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) atakagua Wizara ya Ujenzi na tunaambiwa wakala huo upo chini ya Ofisi ya Rais. Hivi Serikali inataka kuficha nini?”amehoji Zitto.

Lakini jana jioni Jumatatu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika amesema: “Kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, anayegawa majukumu ya kila wizara ni Rais. Rais  atapanga hizo kazi kwa wizara mbalimbali kwa jinsi atakavyoona inafaa.

“Wote tumepangiwa kazi za kufanya na Rais. Hii si mara ya kwanza ni jambo la kawaida. Kwa mujibu wa sheria za mgawanyo wa kazi, kwa jinsi atakavyoona inafaa Rais ndiye mwenye madaraka ya kufanya hivyo.”

 

Aliongeza: “Mfano taasisi ya Tanzania Investment Centre (Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC) imehamishwa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na kupelekwa ofisi ya Waziri Mkuu.

 

“Kama ilivyohamishwa TIC ndivyo alivyofanya kwa wakala wa ndege za Serikali. Hao ATCL (Shirika la Ndege Tanzania) mnaotaka wakabidhiwe ndege zote ndio waliotufikisha nchi hapa tukawa hatuna ndege.”

Advertisement