Wabunge waibua mjadala Hospitali ya Mirembe kujengwa Dodoma, Serikali yatoa ufafanuzi

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile akijibu maswali katika kikao cha 13 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustin Ndugulile ametaja sababu za kujengwa hospitali ya magonjwa ya akili ya Mirembe kwamba hautokani na wenyeji wa Dodoma kuwa na matatizo ya akili

Dodoma. Serikali ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu sababu za kujengwa kwa hospitali ya magonjwa ya akili ya Mirembe jijini Dodoma kuwa haikutokana na mkoa huo kuwa na wagonjwa wengi.

Majibu hayo yametolewa leo Alhamisi Aprili 18, 2019 wakati wabunge walipojadili kuhusu masuala ya magonjwa ya akili swali ambalo liliibua mjadala kwa wabunge.

Akijibu swali hilo ambalo Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa ameliuliza kama utani, akisema mitandao mingi ilikuwa inazungumzia kwa nini maeneo mengine imejengwa miradi wakati Dodoma kuna hospitali ya magonjwa ya akili.

"Si kweli kuwa Dodoma kuna wagonjwa wengi wa akili lakini hospitali ya Mirembe ni hospitali ya rufaa iliyojengwa kwa sababu ya kuwapo wa Gereza Kuu la Isanga ambalo linapokea watu wenye kesi kubwa hivyo huweza kupata msongo (wa mawazo)," amesema Dk Ndugulile.

Katika swali la msingi Mbunge wa Njombe (CCM, Edward Mwalongo aliuliza kama Serikali inawahudumia wagonjwa wa akili wanaozurura mitaani katika masuala ya matibabu, mavazi na makazi.

Naibu waziri amesema Serikali imeendelea kuimarisha afya ya akili kuanzia ngazi za juu hadi ngazi ya msingi ambako jamii inatoka.

Amesema pamoja na idadi kubwa ya wagonjwa wanaorandaranda mitaani, bado huduma zinatolewa lakini akasema sheria ya afya ya akili ya mwaka 2008 inawataka ndugu na jamii kuibua wagonjwa wa akili na kuwapeleka kupata matibabu.