Majaliwa aongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa kitega uchumi CCT

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa kitega uchumi cha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), ambapo jumla ya Sh357 milioni kilipatikana kati ya Sh2 Bilioni zilizotarajiwa kukusanywa.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kupunguza kiwango cha utegemezi kwa washirika wa maendeleo katika bajeti kutoka asilimia 12.8 mwaka 2017/18, hadi asilimia nane kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Majaliwa ameyasema hayo jijini Dodoma leo Ijumaa Julai 5, 2019 wakati wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kitega uchumi cha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Amesema katika mkakati huo wa kuimarika kwa bajeti, kunakwenda sambamba na kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile elimu, maji, na afya, mkakati ambao unaungwa mkono na taasisi za dini.

“Jambo hili la kihistoria mnalolitekeleza sasa la kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kiuchumi, linapaswa kupongezwa sana, Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za CCT ili kufikia hatua muhimu ya kuwahudumia wananchi pamoja na kuunga mkono hatua ya Serikali ya kuwatumikia wananchi kwa sababu jengo hilo litakuwa linatumiwa na jamii nzima ya Watanzania,” amesema Majaliwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCT, Canon Matonya amesema ujenzi wa kitega uchumi hicho Mkoani Dodoma ni  kuunga mkono juhudi za Serikali  kuhamishia makao yake makuu Dodoma.

Matonya amesema zaidi ya Sh14.7 bilioni zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa mradi huo na matarajio katika harambee hiyo yalikuwa ni  kupata Sh2 bilioni.

Amesema fedha nyingine wanatarajia kukopa kwenye taasisi za kifedha zenye masharti nafuu na lengo lao kuondokana na fedha za wafadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.

Katika harambee hiyo, Sh357 milioni zilipatikana.