KESI YA KINA KITILYA: Wakili wa Kitilya adai Serikali ilishinda kesi Uingereza

Friday July 12 2019

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakili wa mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya amedai mahakamani kuwa Serikali ilishashinda kesi katika Mahakama ya Uingereza na kulipwa fidia ya Dola za Marekani 7 milioni, kuhusiana na kesi inayomkabili mteja wake na wenzake wanne.

Wakili huyo, Dk Masumbuko Lamwai alitoa madai hayo huku akiungwa mkono na mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Shose Sinare wakati akimhoji shahidi wa pili katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, Mgonya Benedict kuhusiana na ushahidi wake aliokuwa ameutoa.

Hata hivyo, shahidi huyo ambaye ni kaimu kamishna wa sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, inayohusika na uchambuzi wa awali wa mapendekezo ya mikopo ya Serikali katika kujazia bajeti, alisema hajui kama Serikali ilishalipwa kiasi hicho.

Pia, aliieleza mahakama kuwa hajui chochote kuhusiana mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, wala hakushiriki katika mchakato wowote uliosababisha kesi hiyo.

Mbali na Kitilya na Shose, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Sioi Solomoni. Shose na Sioi walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbick. Wengine ni maofisa wawili wa zamani wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Wote wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwamo ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Dola 6 milioni, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Advertisement

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Immaculata Banzi, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake wa msingi, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya, Lamwai alimhoji shahidi huyo maswali mbalimbali kuhusiana na ushahidi wake huo likiwamo kama anajua kuwa Serikali ilishalipwa kiasi hicho cha fedha.

Awali, Lamwai alimuuliza kama anajua kuwa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo ilihusika kuiwezesha Serikali kupata mkopo huo ikishirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania, ilishairejereshea Serikali Dola za Marekani 6 milioni.

Kabla Lamwai hajamaliza kuuliza swali lake hilo, Shose alimnong’oneza akimweleza kuwa ni Dola 7 milioni naye akarekebisha kwa kurudia kumuuliza huku akitaja kiwango lakini shahidi huyo akajibu kuwa hajui.

“Unajua kuwa Mahakama ya Uingereza ilijadili mahusiano ya Serikali na Standard Bank, na USD (Dola za Marekani) 7 milioni zilirejeshwa na Standard baada ya kutiwa hatiani kuhusiana na mkopo huo baada ya Serikali kudaiwa kuwa iliongezewa ada ya mkopo huo?” aliuliza Lamwai.

Pia alimuuliza shahidi huyo kama anafahamu uhusiano wa kampuni ya Egma, inayomilikiwa na mshtakiwa wa kwanza (Kitilya) na Serikali, Egma na benki za Stanbic na Standard, kuhusiana na mikataba na makubaliano ya malipo, lakini maswali yote alisema kuwa hajui.

Shahidi huyo pia alijibu kuwa hakuhusika katika mchakato wowote wa mkopo huo na wala hakukaa katika kamati yoyote ya wizara iliyohusika kujadili na kupitisha mapendekezo ya mkopo, kwani wakati huo hakuwa mjumbe kwenye kamati yoyote.

Alipoulizwa nini anachokijua kuhusiana na kesi hiyo ambacho alikwenda kukithibitisha mahakamani, alijibu kuwa ni kueleza tu kazi za idara ya sera.

Akijibu maswali ya wakili Charles Alex anayewatetea Shallanda na Missana, shahidi huyo alisema mapendekezo yaliyotolewa na kamati mbili za wizara hiyo zinazohusiana na usimamizi wa madeni; kwenda kwa waziri kuhusu mkopo yalikuwa ya kamati na si mtu mmoja.

Lakini alipoulizwa kama anajua chochote kuhusiana na mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao pia alisema hajui.

“Shahidi utakubaliana na mimi kuwa wewe kama binadamu na kwa nafasi yako hujui chochote kuhusiana na makosa au mashtaka haya?” aliuliza wakili Alex lakini shahidi akakaa kimya.

“Sema tu ukweli wako mbele ya Mungu.”, wakili huyo alimsisitiza ajibu swali lake ndipo shahidi huyo kwa sauti ya unyonge na ya chini akajibu, “nakubaliana na wewe.”

Kwa kiasi kikubwa shahidi huyo alipata wakati mgumu kujibu maswali ya mawakili wa utetezi kwani mengine alikuwa anatumia muda mrefu kabla ya kuyajibu na alikaa kimya kwa mengine hadi pale mawakili walipolazimika kuyarudiarudia. Wakati mwingine ilimlazimu Jaji Banzi kuingilia kati kumwelekeza ajibu.

Baada ya kuhojiwa na mawakili hao wa utetezi, shahidi huyo aliulizwa tena maswali na wakili wa Serikali, Tibabyekomya kwa lengo la kusawazisha maswali aliyokuwa ameulizwa na mawakili ambayo yalionekana kumpa wakati mgumu kuyajibu.

Katika maswali hayo ya kusawazisha majibu ya maswali ya mawakili, shahidi huyo alifafanua kuwa hajui kama pesa hizo alizoulizwa na wakili Lamwai zilishalipwa na benki ya Standard kwa Serikali kwa kuwa idara ya sera anakofanya kazi yeye haihusiani na malipo.

Alieleza kuwa idara hiyo inahusiana na uchambuzi wa awali tu wa mapendekezo ya kuikopesha Serikali yanayowasilishwa na taasisi mbalimbali za kifedha na kwamba suala la malipo linamhusu mhasibu mkuu wa wizara hiyo ambaye ndiye huyapokea malipo yote.

Awali, katika ushahidi wake wa msingi shahidi huyo alieleza kuwa kabla ya nafasi hiyo ya ukaimu kamishna wa sera, alikuwa mchumi mkuu wa idara ya sera, tangu mwaka 2009 hadi mwaka 2017 alipokaimishwa nafasi hiyo na kueleza muundo na majukumu ya idara hiyo.

Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa miongoni mwa majukumu yake ni kutafuta vyanzo vya fedha ili kujazia upungufu katika Bajeti ya Serikali na kwamba vyanzo hivyo ni pamoja na mikopo ikiwamo ya masharti nafuu.

Alisema kila mwaka baada ya bajeti kupitishwa taasisi mbalimbali za kifedha huwa zinawasilisha wizarani kwa katibu mkuu au kwa waziri, mapendekezo ya kuikopesha Serikali ili iweze kutekeleza miradi yake ya maendeleo.

Alisema mapendekezo hayo baada ya kupokewa na ama katibu mkuu au waziri, huyapaleka katika idara ya sera, ambayo ndiyo husimamia madeni. Huko, alisema kuna wataalamu wa wizara ambao hufanya uchambuzi wa awali. Baada ya uchambuzi huo, sekretarieti ya wataalamu hupeleka uchambuzi wake na mapendekezo kwa Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Madeni (TDMC), ambayo mwenyekiti wake ni kamishna wa sera.

TDMC ambayo inaundwa na wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali kutoka Bara na Zanzibar, baada ya kufanya uchambuzi hutoa mapendekezo ambayo hupelekwa Kamati ya Taifa ya Usimamizi wa Madeni (NDMC) ambayo pia huundwa na wakuu wa taasisi na idara mbalimbali za Serikali ya Bara na Zanzibar zikiwamo za kifedha ambayo mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, na Katibu wake ni Kamishna wa Sera na ndio humshauri waziri wa fedha kuhusu mikopo ndani na nje ya nchi. Hivyo alisema baada NDMC kupitia uchambuzi na mapendekezo ya TDMC, hupeleka uchambuzi na mapendekezo yake kwa waziri wakieleza kuridhika au kutokuridhika na masharti na taarifa nyinginezo kuhusu mkopo huo na ndipo waziri anaidhinisha au kutokuidhinsia ukopaji huo.


Advertisement