Kilichojificha shule 10 bora matokeo ya kidato cha sita

Katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la mitani (NACTE)  Charles Enock Msonde ikifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari mjini Ungu leo wakati alipokua akitoa taarifa ya matukio ya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2019. Picha na Muhammed Khamis 

Dar es Salaam. Hazijashika nafasi ya kwanza, ya pili wala ya tatu kwa ubora kitaifa, lakini ndizo shule zenye watahiniwa wengi waliopata daraja la kwanza.

Moja imeshika nafasi ya sita nyingine nafasi ya nane. Hizi ni shule za Kibaha na St Mary’s Mazinde Juu ambazo kwa mujibu wa taratibu za upangaji wa ubora wa shule zimeangushwa na wastani mdogo wa ufaulu wa masomo kwa jumla.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema ubora wa shule unapimwa kwa kuangalia wastani wa ufaulu wa kila somo na kugawanya na idadi ya wanafunzi.

“Tunaangalia ubora wa kila somo na kugawanya kwa idadi ya shule husika ndiyo tunapata shule zilizoshinda,” alisema.

Uchambuzi madaraja shule kumi bora

Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotangazwa juzi yanaonyesha Shule ya Kasimiri iliyopo mkoani Arusha kuongoza katika shule 10 bora.

Katika matokeo hayo, Kisimiri imefuatiwa na Feza Boys ya Dar es Salaam, kisha Ahmes ya Pwani, Mwandet ya Arusha na Tabora Boys ikishika nafasi ya tano. Kisimiri ilikuwa na watahimiwa 60 ambao ni theluthi ya wanafunzi wa St Mary’s Mazinde Juu iliyokuwa na watahiniwa 217 na Kibaha watahiniwa 172.

Wakati Kisimiri ikibebwa na idadi ndogo ya wanafunzi huku watahiniwa 58 wakipata daraja la kwanza, Mazinde pamoja na kuwa na daraja la kwanza 176 na Kibaha 143, uchambuzi unaonyesha wingi wa wanafunzi na tofauti za watahiniwa katika madaraja mengine yamechangia kuziteremsha.

Kisimiri ina watahiniwa wawili tu waliopata daraja la pili, na kufanya jumla ya watahiniwa kuwa 60, haina watahiniwa waliopata daraja la tatu, la nne wala sifuri.

Mazinde ambayo ndio kinara kwa kuwa na daraja la kwanza ina daraja la pili 38 na daraja la tatu wanafunzi wawili. Kibaha kwa upande wake ina daraja la kwanza 143, la pili 26 na la tatu wanafunzi watatu.

Shule nyingine zilizobebwa na uchache wa wanafunzi na kuzifanya ziingie 10 bora ni pamoja na Ahmes ya Bagamoyo mkoani Pwani ambayo imeshika nafasi ya tatu kitaifa.

Shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 99 waliopata daraja la kwanza ambayo ni sawa na asilimia 88, huku 13 wakipata daraja la pili, wakati shule ya sekondari ya Tabora Boys iliyoshika nafasi ya tano ikifuatia kwa kuwa na wanafunzi 87 waliopata daraja la kwanza sawa na asilimia 82, huku wanafunzi 19 wakipata daraja la pili.

Nyingine ni Feza Boys iliyoshika nafasi ya pili ina wanafunzi 72 waliopata daraja la kwanza, 15 wakipata daraja la pili, huku Shule ya Mwandet ya Arusha iliyoshika nafasi ya nne ina wanafunzi 70 waliopata daraja la kwanza na sita wamepata daraja la pili.

Nyingine ni Canossa ya Dar es Salaam ikiwa na wanafunzi 64 wenye daraja la kwanza na 19 wenye daraja la pili.

Shule ya Feza Girls (Dar es Salaam) nayo ina wanafunzi 54 wenye daraja la kwanza, 12 wenye daraja la pili, huku shule ya sekondari ya Kemebosi iliyoshika nafasi ya 10 ikiwa na wanafunzi 26 na wanafunzi saba wenye daraja la pili.

Shule nyingine zinazoonekana kuponzwa na idadi kubwa ya wanafunzi na ufaulu wa masomo ni pamoja na Ilboru ya Arusha ambayo licha ya kutokuwamo kwenye 10 bora, ina wanafunzi 129 wenye daraja la kwanza sawa na asilimia 74, wanafunzi 42 wenye daraja la pili na watatu wenye daraja la tatu.

Nyingine ni sekondari ya Weruweru ya mkoani Kilimanjaro iliyoshika nafasi ya 143, ina wanafunzi 116 wenye daraja la kwanza, 169 wenye daraja la pili na 94 wenye daraja la tatu.