Magufuli atoa siku saba kwa wizara ya ujenzi, Tanroads

Rais John Magufuli

Muktasari:

Daraja la Kigongo-Busisi litakalounganisha wilaya za Misungwi na Sengerema lenye urefu wa kilomita 3.2 litakuwa ndilo refu kuliko zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameipa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) muda wa wiki moja kuanzia Julai 15, 2019 kutia saini makubaliano ya mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2.

Daraja hilo litakalokuwa refu kuliko yote ya Afrika Mashariki na Kati linajengwa juu ya Ziwa Victoria kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni zinazotokana na fedha za mapato ya ndani na litaunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza.

Akihutubia wananchi jijini Mwanza jana jioni Jumatatu Julai 15, 2019 wakati wa hafla ya kuzindua huduma mbalimbali za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Rais Magufuli pia ametoa muda wa miezi miwili kwa mkandarasi atakayetekeleza mradi huo kukusanya vifaa tayari kuanza ujenzi.

“Kila siku watu wamekuwa wakisubiri feri (kwa muda mrefu)...haiwezekani kila siku tunategemea feri. Unafika pale mama mjamzito mpaka ukasubiri feri; uchungu utakusubiri? (wakati) Mtoto anataka atoke. Pale wameshakufa watu. Tumeomba fedha (kutoka kwa wafadhili) tumekosa. Tumeamua tunajenga kwa fedha zetu wenyewe,” alisema Rais Magufuli

“Tumetenga Sh700 bilioni na mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kujenga daraja reli kuliko yote Afrika Mashariki na Kati,” alisema

Ujenzi wa daraja hilo siyo tu litawapunguzia wananchi adha ya kutumia muda mrefu kusubiri huduma ya vivuko viwili vya Mv Mwanza na Mv Misungwi zinazotoa huduma eneo la kivuko cha Kigongo-Busisi, bali litachangamsha shughuli za kiuchumi katika mikao ya Kanda ya Ziwa, hasa Mwanza, Geita na Kagera.

Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) mkoa wa Mwanza, Kalonda Hassan alisema wasafiri wanaovuka eneo hilo hulazimika kutumia wastani wa kati ya dakika 30 hadi 40 kupata huduma nyakati za mchana na dakika 60 hadi 80 usiku kulingana wingi wa abiria na magari yanayovushwa.

Akitoa maelezo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elius Kwandikwa, Mkuu wa Kivuko cha Kigongo-Busisi, Abdallah Atiki alisema vivuko vya Mv Mwanza na Mv Misungwi husafirisha kati ya abiria 6,500 hadi 8,000 na magari 730 kwa siku.

Mkoa wa Mwanza una vivuko 10 vinavyotoa huduma ya kusafirisha abiria, magari na mizigo kati ya maeneo mbalimbali katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na visiwa vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria.

Kivuko kipya cha Mv Mwanza ndicho chenye uwezo wa kubeba tani 250 ikiwa ni pamoja na abiria 1, 000, mizigo na magari 36 kwa wakati ndicho kikubwa kuliko vyote ndani ya Ziwa Victoria.