Serikali ya Tanzania yaweka ulinzi kitalu ilichokifuta cha Green Mile Safaris

Muktasari:

Mgogoro wa umiliki wa  Kitalu cha uwindaji wa Kitalii cha  Lake Natron,(east) kilichopo wilayani Longido mkoani Arusha nchini Tanzania umeendelea na sasa Serikali ya Tanzania imechukua udhibiti wa eneo la kitalu kwa kuweka ulinzi.

Arusha. Serikali ya Tanzania imechukua udhibiti wa kitalu cha uwindaji  wa kitalii cha  Lake Natron (EAST) kilichokuwa kinamilikiwa na kampuni ya Green Mile Safaris Ltd.

Uamuzi huo unafuatia baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla kutangaza kuiondoa kampuni hiyo kumiliki kitalu hicho, kutokana na migogoro baina ya wananchi, halmashauri na Serikali ya Longido mkoani Arusha dhidi ya kampuni hiyo.

Uamuzi kama huu, pia uliwahi kuchukuliwa mwaka 2004 pale alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipoinyang'anya kampuni hiyo kitalu hicho kutokana na kukiuka taratibu za uwindaji.

Hata hivyo, kampuni hiyo, ilikwenda mahakamani kupinga uamuzi huo na baada ya mgogoro wa muda mrefu, baada ya Nyalandu kuondolewa nafasi hiyo, aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Profesa Jummane Maghembe aliirejeshea kitalu kampuni hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 9,2019, Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema kitalu hicho kipo chini ya udhibiti wa Serikali na kampuni hiyo imepewa muda wa kuondoa baadhi ya vitu vyake.

"Ni kweli baada ya uamuzi wa Waziri (Kigwangalla) hiki kitalu kinalindwa na vyombo vya Serikali na kuna maelekezo wamepewa kuondoka," amesema

Amesema kwa muda mrefu kampuni hiyo, imekuwa ikilalamikiwa na vijiji 23 kutokana na kukaidi kulipa malimbikizo ya madai kiasi cha Sh336 milioni.

Maofisa tarafa za Longido, Kitumbeine na Ngarenaibu  jana Alhamisi pia walitembelea kitalu hicho ili kuwaeleza rasmi watendaji wa kampuni hiyo, uamuzi wa kutakiwa kuondoka.

Ofisa Tarafa wa Longido, Erick Nyalinga amesema walifika katika kitalu hicho, kufikisha ujumbe wa Serikali kuhusu kusitishwa shughuli za kampuni hiyo.

Amesema mali zinazomilikiwa na kampuni hiyo, zitakuwa chini ya mamlaka za Serikali hadi pale kampuni hiyo, itakapolia kiasi cha Sh336 milioni zinazodaiwa na vijiji 23.

Hata hivyo, kampuni ya Green Mile imepinga uamuzi wa waziri kuondolewa katika kitalu hicho, kwa maelezo kuwa taratibu hazikufuatwa.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Awadhi Abdallah ameeleza kuna taratibu za kufuata katika kufuta kitalu na kuna mamlaka za kukata rufaa.

Amesema mgogoro umekuja sasa wakati bado wana kesi mahakamani kuhusiana na migogoro ya Kitalu hicho lakini pia wamemshitaki kesi ya madai Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe kwa kuwaharibia biashara.