ACT Wazalendo chatoa maoni taulo za kike

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo  Zitto Kabwe akizungumza na wandishi wa habari kuhusu bajeti ya Taifa

Muktasari:

  • Chama hicho kimesema mipango makini inahitajika kuvutia wawekezaji watakaotengeneza taulo hizo ili kuwasitiri wanawake.

Dar es Salaam. Baada ya Serikali kupendekeza kurudisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike, chama cha ACT Wazalendo kimetoa ushauri jinsi ya kushughulikia suala hilo kwa manufaa zaidi.

Hayo yamesemwa leo, Juni 16, 2019 na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alipokuwa anachambua bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20 ambayo iliwasilishwa Alhamisi iliyopita.

Zitto amesema kurejesha VAT kwenye taulo hizo ni sawa na kuwalipisha zaidi ya wanawake wote wanaoingia hedhi kila mwezi nchini.

"Hedhi ni suala la kibailojia sasa kirudisha VAT kwenye taulo hizo ni kuwalipisha wanawake kwa suala lililo nje ya uwezo wao," amesema Zitto.

Kuondokana na hali hiyo, Zitto amesema Serikali ipitishe bei elekezi kwa bidhaa hizo ili kuwadhibiti wafanyabiashara wanaoelezwa kunufaika zaidi na msamaha uliokuwa umetolewa.

Biashara ya taulo hizo, ACT Wazalendo kimesema ni ya thamani ya Dola 150 milioni inayowanufaisha zaidi ya wanawake milioni 12 wanaoingia hedhi kila mwezi hivyo, inahitaji usimamizi zaidi kwani sehemu yenye mianya ya kujinufaisha ni usambazaji.