AJALI YA MOROGORO: Wenye malori watoa msaada wa vifaa vya Sh20 milioni Muhimbili

Wednesday August 14 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) kimetoa msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya majeruhi wa ajali  iliyotokana na lori lililoanguka na kuwaka moto mkoani Morogoro.

Jumla ya vifaa tiba vyenye thamani ya Sh20 milioni vimekabidhiwa leo Jumatano Agosti 14,2019 kwa uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ambapo majeruhi hao wanapatiwa matibabu.

Makamu mwenyekiti wa Tatoa, Elias Lukumai amesema chama chao kimeguswa na tukio hilo ambalo limekatisha maisha ya vijana wengi.

Amesema kwa umoja wao walichangishana fedha ambazo wamezitumia kununua vifaa tiba hivyo walivyopewa maelekezo na madaktari.

“Kama Rais (wa Tanzania, John Magufuli) alivyosema hilo ni janga kubwa hivyo tumeona tuungane na Serikali katika kuhakikisha majeruhi wanapata matibabu na kupona.”

“Tumezungumza na madaktari wakatupa orodha ya vifaa vinavyohitajika na ndiyo hivyo tumeleta tunawaomba na wengine wajitokeze,” amesema Lukumai

Advertisement

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utasishaji, Batusaje John amesema vifaa vilivyokabidhiwa ni muhimu katika matibabu ya majeruhi wa moto hivyo ni msaada mkubwa kwao.

Ajali hiyo ilitokea Jumamosi iliyopita ya Agosti 10, 2019 eneo la Msamvu mkoani Morogoro ambapo hadi leo vifo vilivyoripotiwa ni 81 na majeruhi zaidi ya 40 ambao wamelazwa MNH na wengine Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Advertisement