VIDEO: Agizo la Lugola kwa polisi kuhusu bodaboda zilizokamatwa Tabora

Monday May 20 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akijibu

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora  limepewa saa kadhaa leo asubuhi Jumatatu Mei 20, 2019 kuziachia pikipiki zote walizozikamata na ikifika jioni bila agizo hilo kutekelezwa,  watakumbana na mkono wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Kauli hiyo imetolewa na Lugola leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum (CUF), Rehema Migilla.

"Nilishatoa maagizo kwa nchi nzima kuwa bodaboda zinazotakiwa kupelekwa polisi ni kwa makundi maalumu lakini sio kila kosa,  sasa kama Tabora wanashikilia pikipiki naagiza hadi jioni wawe wamezitoa kwa wahusika vinginevyo ama zao au zangu," amesema Lugola.

Lugola ametaja makosa ya pikipiki kutakiwa kupelekwa kituo cha polisi kuwa ni kesi za uhalifu, zinazoibiwa na zisizo na wenyewe na kwamba makosa mengine ni ya kulipa faini.

Katika swali la msingi Migilla alitaka kujua ni kwa nini pikipiki zinazokamatwa na kupelekwa vituoni zinaibiwa vifaa ikiwemo betri.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,  Hamad Masauni amesema sheria ya usalama barabarani sura ya 168 inampa askari mamlaka ya kusimamisha chombo chochote  barabarani na kukikagua kama kina makosa ana uwezo wa kukizuia.

Advertisement

Amesema wanapobaini kielelezo kimeharibika, uchunguzi hufanyika na hatua huchukuliwa kwa waliohusika na upotevu huo.

Advertisement