Agizo la Magufuli, lawafutia kesi ya mauaji

Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP) Biswalo Mganga

Muktasari:

  • Waliotuhuniwa kwa mauaji wafutiwa mashitaka baada ya Rais John Magufuli kusoma barua yao katika moja ya gazeti la kila siku.

Dodoma. Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP) Biswalo Mganga amewafutia shitaka la mauaji watuhumiwa Musa Sadiki na Edward Matiku baada ya agizo la Rais John Magufuli.

Mganga amewaambia waandishi wa habari leo Alhamisi Machi 14, 2019 kuwa, Rais Magufuli alitoa maagizo ya kuchunguzwa kwa kesi hiyo baada kusoma habari za Musa Sadiki kupitia vyombo vya habari.

Machi 6, 2019 mahabusu huyo aliandika barua kwa wasomaji katika moja ya gazeti la kila siku ikionyesha namna alivyobambikiwa kesi ya mauaji na polisi huku wakichukua vitu vyake ikiwemo fedha taslim Sh788,000 na simu ya mkononi.

"Rais alisoma barua hiyo na kunitaka nifuatilie ukweli, nimechunguza na kufika gerezani na kituo cha polisi, nimejiridhisha maelezo ya mtuhumiwa gazetini ni ya kweli, yeye na mwenzake nimewafutia mashitaka na ninaagiza mali zao kurejeshwa mara moja," amesema Mganga.

DPP ameagiza jeshi la polisi kuwachunguza waliohusika katika kupanga kesi hiyo namba 8/2018 mkoani Tabora ili wachukuliwe hatua huku akiweka sharti la kesi zote za jinai kupitia ofisi yake kabla ya kwenda mahakamani.