Agizo la Magufuli kontena zilizokwama bandarini lafanyiwa kazi

Saturday July 20 2019

 Fedha na Mipango,Wizara Ujenzi, Uchukuzi,Bandari  Dar es Salaam,Kontena saba, vifaa  ,ujenzi ukarabati ,meli Mv Victoria , Mv Butiama,

 

By Ngollo John, Mwananchi [email protected]

Mwanza.  Kontena saba kati ya 56 za vifaa vya ujenzi na ukarabati wa meli za Mv Victoria na Mv Butiama zilizokuwa zimekwama Bandari ya Dar es Salaam  zinatarajiwa kuwasili jijini Mwanza leo Jumamosi Julai 20, 2019.

Julai 16, 2019 Rais wa Tanzania, John Magufuli aliwabana makatibu wakuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Fedha na Mipango kuhusu kukwama kwa vifaa hivyo katika bandari hiyo.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi aliagiza vifikishwe Mwanza kwa ajili ya ukarabati na ujenzi huo, kuwaagiza watendaji hao kukaa pamoja kumaliza taratibu zinazotakiwa.

Akizungumza na Mwananchi leo kaimu ofisa habari wa  kampuni ya huduma za meli nchini (MSCL),  Edmund Rutta amesema kontena hizo ni za vifaa vya ujenzi wa chelezo na ukarabati mkubwa wa meli za Mv Victoria na Butiama.

“Zinakuja kwa awamu, zipo zitakazowasili kesho au keshokutwa,” amesisitiza.

Ofisa huyo amesema kuwasili kwa kontena za vifaa hivyo unatokana na agizo la Rais Magufuli.

Advertisement

Ujenzi wa chelezo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh36 bilioni huku ukarabati wa meli ya Mv Victoria ukitarajiwa kuwa Sh22 bilioni na Mv Butiama Sh5 bilioni

Akizungumzia ujenzi wa meli mpya, amesema utagharimu zaidi ya Sh89 bilioni  na kwamba vifaa vyake ambavyo ni kontena 300 vinavyotarajiwa kutoka Korea Kusini vitawasili mwishoni mwa Agosti, 2019.

Viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano,  Isack Kamwele,  naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji, makatibu wakuu wa wizara hizo pamoja na Meneja  Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) watakuwepo kupokea kontena hizo leo.


Advertisement