Ali Kiba ampa ofa aliyemlilia kwenye Fiesta

Tuesday December 25 2018

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku mbili tangu dada anayejulikana kwa jina la Emiliana Mgema kumlilia msanii Ali Kiba akiwa anaimba katika tamasha la Tigo Fiesta, hatimaye msanii huyo amemuona na kutoa ofa kwake.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Ali Kiba alitangaza ofa hiyo huku akiwa ameweka video ya dada huyo akiwa anahojiwa huku analia na kueleza hisia zake jinsi anavyompenda msanii huyo.

Kiba aliandika “Asante sana dada anayemjua huyu dada amwambie nina tiketi yake ya bure na mofaya zake za kutosha tarehe 29 /12 Next Door Arena,” aliandika Kiba wakati anatangaza ofa hiyo kwa Emilina ambapo anatarajia kufanya shoo yake aliyoipa jina la ‘Funga mwaka na KingKiba.’

Mwananchi leo Jumanne Desemba 25,2018 imemtafuta Emiliana ili kujua namna alivyopokea ofa hiyo ambaye amesema, “Nimefurahishwa sana japokuwa hata kama asingenipa ofa nilikuwa nimeshapanga kwenda.”

Hata hivyo, amesema kwa furaha aliyokuwa nayo baada ya Ali Kiba kumtambua na kumpa ofa hiyo, sasa badala ya kwenda usiku atafika saa nne asubuhi ili kuweza kuwahi nafasi ya mbele.

Katika hatua nyingine amewataka mashabiki waelewe kwamba anampenda Ali Kiba kwa kazi yake ya muziki na si vinginevyo kama wanavyofikiria na kuahidi kwamba siku ya onyesho lake kama atakwenda na mkewe pia atamwambia hilo ili asije akawa na wasiwasi naye.

Advertisement

Emy amesema ameanza kumpenda Ali Kiba tangu alipotoa kibao chake cha Macmuga ambapo kipindi hicho alikuwa akisoma darasa la saba Shule ya Msingi Nata mkoani Tabora na kuanzia hapo amekuwa akimfuatilia hadi leo na hakuna ngoma yake hata moja aliyowahi kuiona mbaya.

Advertisement