Alichokisema Barnaba kuhusu afya ya uzazi

Msanii Barnabasi akichngia wakati wa Mdahalo ulioandaliwa na Plan International jijini Dar es Salaam leo kuhusu namna ya usawa wa kijinsia unavyoweza kuleta maendeleo

Muktasari:

Hatua ya kuwafungia watoto kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita kwa madai ya kuwalinda huwapoteza wakati wanapoanza elimu ya juu baada ya kukutana na uhuru uliopitiliza.

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa kizazi kipya Elias Barnaba maarufu kwa jina la Barnabas amesema elimu ya jinsia na afya ya uzazi inapaswa kufundishwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa sababu wengi huangamia na kupoteza malengo yao wakiwa ngazi hiyo ya elimu.

Amesema wanafunzi wengi hawakuwahi kukutana na uhuru uliopitiliza shule za msingi na sekondari ndio maana wanapofikia ngazi hiyo kielimu hujiachia bila tahadhari.

Akizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Shirika la Plan International juu ya namna usawa wa kijinsia unavyoweza kuchochea maendeleo,  Barnabas amesema siku hizi wasichana na wavulana wenye umri mdogo wanafika elimu ya juu bila kuwa na uzoefu wa kutumka uhuru.

Amesema kutokana na hali hiyo elimu ya afya na usawa wa kijinsia inapaswa kufundishwa zaidi vyuo vikuu.

"Unajua shule na msingi hadi kidato cha sita watoto wengi wanabanwa au na wazazi ama shuleni lakini chuo kikuu anajiachia, anajiachia wakati hajui kutumia uhuru huo," anasema Barnabas na kuongeza;

"Ndio maana wengine wanashika mimba nje ya muda sahihi wa kuzaa, elimu isiwasahau hasa."

Awali mchambuzi wa masuala ya kijinsia Richard Mabala amesema tatizo kubwa ni kuwa watoto hawaandaliwi ila wanafunzishwa kufaulu mitihani tu.

"Kwa lugha nyingine watoto wanatahinika na sio kuelimika,mtoto tangu shule ya msingi yupo ndani ya ukuta  na ghafla anafika chuo kikuu na kukuana na uhuru, hili tatizo," amesema Mabala