Alichokisema Magufuli mbele ya Rais Ramaphosa

Rais John Magufuli akimpongeza Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa alipokamilisha hotuba yake katika kongamano la biashara la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lililofanyika katika Ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano cha Mwalimu Nyerere  jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameendelea kusisitiza nchi za Tanzania na Afrika Kusini zijikite katika kuendeleza na kuimarisha mazingira ya ujenzi wa viwanda ili kutengeneza ajira na kuacha kuuza bidhaa ghafi kwa nchi zingine.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amezitaka nchi za Tanzania na Afrika Kusini kujikita katika ujenzi wa viwanda huku akifungua milango kwa wanaotaka kujenga viwanda nchini na kuweka wazi hali halisi ya sasa kiuwekezaji.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 15, 2019 wakati wa mkutano wa baraza la wafanyabiashara wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lililokutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini.

Katika baraza hilo, limehudhuriwa pia na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, mawaziri wan chi hizo mbili pamoja na wafanyabiashara.

Mafuguli ameyataja maeneo ambayo wawekezaji kutoka nchi hiyo wanaweza kuwekeza ikiwemo ujenzi wa viwanda vya nguo, mazao yatokanayo na nyama, samaki, viwanda vya magari, viwanda vya dawa na maeneo mengine.

Amesema lengo ni kupunguza bidhaa ghafi zinazokwenda nje ambazo zikiachwa katika nchi husika zitaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana.

“Tunahitaji kutengeneza nguo kwa pamba zetu na Tanzania ni ya pili kuwa na mazao ya nyama ikiongozwa na Ethiopia, tutaweza kuzalisha viatu na bidhaa zingine zitokanazo na ngozi, tunao samaki katika bahari na maziwa yetu, lengo kufikia mahali ambapo tunaweza kuzalisha bidhaa zetu hapahapa ndani ya nchi. Milango iko wazi kwa ajili ya uwekezaji,” amesema.

Akizungumza suala la kukuza viwanda na uwekezaji, Rais Magufuli amesema mifumo wezeshi inawekwa ili kuwezesha Tanzania ya viwanda akiitaja miradi kadhaa ikiwemo nishati katika bonde la Rufiji, ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, reli, anga.

“Tumeweza kufufua shirika letu la Air Tanzania na hivi sasa kuna ndege inayotoka hapa nchini na kwenda Afrika Kusini mara nne kwa wiki, hii itasaidia kuwezesha biashara na uwekezaji lakini pia kukuza  utalii wa ndani kati ya nchi zetu mbili, lakini pia bandari zinatanuliwa na kujengwa,” amesema.

Aidha Magufuli amesema Afrika Kusini imefanikiwa kuwekeza katika makampuni 228 nchini Tanzania na kuzalisha ajira zipatazo 21,075 na hivyo kuwa nchi ya 13 yenye uwekezaji mkubwa kiuchumi ndani ya nchi.