VIDEO: Alichokisema Mbowe bungeni hiki hapa

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amedai huenda kesi za utakatishaji fedha ni mkakati mpya wa kukuza mapato ya Serikali. Ametoa kauli hiyo leo jioni Ijumaa Aprili 12, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) bungeni jijini Dodoma.

Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Tanzania, Freeman Mbowe amesema kwa sasa inaonekana kama kesi za utakatishaji fedha ni mkakati mpya wa kukuza mapato ya Serikali.
Mbowe ametoa kauli hiyo  Ijumaa Aprili 12, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mwaka 2019/2020.


Mbowe aliwema: “Imekuwa utamaduni wa Serikali kugeuza kesi za utakatishaji fedha kama chanzo cha mapato.


“Yaani inaonekana kama kesi hizi ni mkakati mpya wa kukuza mapato ya Serikali. Watu wanakamatwa, uchunguzi unaendelea miezi sita au mwaka mzima na Magereza Dar es Salaam zimejaa mahabusu zaidi ya 5,000.”


Amesema mahabusu hao kesi zao zinaendelea na hawapewi haki huku baadhi wakiwa hawajui hata mashtaka yao. “Wanawarundika watu ambao walipaswa kuwa nje kwa misingi ya dhamana.”


Mbowe amesema baadhi ya watu wanaokamatwa ni mabosi wa mashirika makubwa ambayo yanachangia mapato kwa Serikali.
“Wengine wanaoshitakiwa kwa makosa ya rushwa ni watu ambao wapo katika miradi ya PPP (ubia kati ya sekta binafsi na Serikali). Leo Mkurugenzi wa shirika la Usafiri Dar es Salaam, mke wake na viongozi wa shirika hilo wapo mahabusu kwa kesi ya utakatishaji fedha.


“Na huyu ni mbia wenu mngeweza kukaa katika vikao vya bodi na kumalizana  naye. Tukiendelea na utaratibu huu ni nani atakuwa na uwezo wa kuwekeza na Serikali wakati  Serikali inawaweka ndani wabia wake?


Vyama vya siasa kuminywa
“Ukiuliza Serikali imezuia kazi za vyama vya siasa kwa sheria gani hakuna jibu. Nyinyi mnaona sifa kwamba mtashinda uchaguzi wakati mnazuia vyama va siasa visifanye kazi yake ya kikatiba,” amesema Mbowe.
“Maisha ya siasa ni ya kila siku mnazuia vyama vya siasa harafu mnasema tunawashinda wapinzani, mnaogopa nini Ruhusuni tufanye kazi ya siasa, mnatufunga mikono harafu mnalinga hapa tuache tukafanye siasa.”


Tume huru ya Uchaguzi
Mbunge huyo wa Hai amegusia pia uwepo wa tume huru ya uchaguzi, akibainisha kuwa uwepo wake ni jibu tosha la utawala bora,  akifafanua kuwa hata kiongozi akishinda atatembea kifua mbele akijua kuwa ameshinda kwa haki, si kama ilivyo sasa watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wanateuliwa na Rais.