Alichokisema Waziri Kakunda kuhusu bidhaa bandia Tanzania

Friday January 11 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda ameitaka Tume ya Ushindani  Tanzania (FCC) kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia.

Pia ameitaka tume hiyo kuingia makubaliano na Serikali ya China ili kuwasaidia kuthibiti ubora wa bidhaa zinazoingia zinazotoka nchini humo kabla ya kuingia Tanzania.

Waziri Kakuda ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Januari 11, 2019 alipotembelea tume hiyo kwa ajili ya kujifunza shughuli zinazofanywa na tume hiyo na kuzungumza na watumishi wake.

"Ushindani usio wa haki uko ndani ya mishipa ya binadamu hususan wafanyabiashara hivyo tunapaswa kuongeza nguvu zaidi. Lazima tuwalinde wawekezaji wa kweli, lazima tulinde mitaji yao. Pekee yenu hamuwezi lazima mshirikiane na mamlaka nyingine vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama," amesema Kakunda.

Amesema katika mkoa wa Pwani na Kagera wakuu wake wa mikoa wanafanya vizuri kudhibiti bidhaa bandia, kwamba anatamani kuona FCC inashirikiana na makamishna wa mikoa yote.

"Tatizo kubwa lililopo ni kufungasha mara ya pili ili kukwepa tarehe ya bidhaa fulani kuharibika au kukwepa kodi kwani bidhaa nyingine zinakuwa zimeingia nchini kinyemela," amesema

"Katika utekelezaji wa mambo haya busara inahitajika lakini msiwe wepesi wa kukubali mambo ya 'Repackaging' (kufungasha kwa mara nyingine).”

Ameongeza, “Mtu akikutwa anatengeneza vifungashio hana taarifa muhimu  inayoonyesha oda mzalishaji husika achukuliwe hatua.”

 

 

 


Advertisement