Amber Rutty kusomewa maelezo ya awali Machi 7

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 7, 2019 kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa Rutyfiya Abubakary maarufu 'Amber Ruty' na wenzake wawili.

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Machi 7, 2019 kumsomea maelezo ya awali

mshtakiwa Rutyfiya Abubakary  'Amber Ruty' na wenzake wawili.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Februari 11, 2019  na Hakimu Mkazi , Augustine Rwezile baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Amber Rutty na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kufanya mapenzi kinyume na maumbile, katika mahakama hiyo.

Wakili wa Serikali, amedai kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea Maelezo ya awali.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wa shauri hilo, umekamilika hivyo tunaomba terehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea Maelezo ya awali," amedai Nguka.

Nguka baada ya kueleza hayo, Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 7, 2019.

Mbali na Amber Rutty, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Said Mtopali na James Charles maarufu kama 'James Delicious'.

Washtakiwa hao walifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza Novemba 2, 2018 wakikabiliwa na kosa la kufanya mapenzi kinyume na maumbile.

Katika kesi hiyo kosa la kufanya mapenzi kinyume na maumbile linamkabili Amber Ruth na anadaiwa amelitenda kati ama baada ya Octoba 25, 2018 ambapo alimruhusu Said Bakary kumuingilia kinyume na maumbile, kosa ambalo amelikana.

Pia kosa jingine la kufanya mapenzi kinyume na maumbile, linamkabili mshtakiwa wa pili Said Bakary ambapo anadaiwa kati ama baada ya Oktoba 25,2018 jijini Dar es Salaam alifanya mapenzi na Amber Rutty kinyume na maumbile ambapo alisema si kweli.

Kosa la tatu la kuchapisha video ama picha za ngono, linalomkabili James Charles au James Delicious akidaiwa kati ya Oktoba 25, 2018 alisambaza video za ngono kupitia makundi ya Whatsapp.

Kosa jingine la nne ni kusababisha kusambaa picha za ngono linamkabili Amber Ruth na Said Aboubakary ambapo wanadaiwa kati ya Oktoba 25, 2018 walisababisha kusambaza picha za ngono kupitia makundi ya Whatsapp. Kosa ambalo wamelikana.