Amnyonga mtoto baada ya kuwadai wazazi Sh10 milioni za ‘kumkomboa’

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mtoto Junior Siame (8)wakitoka nyumbani mtaa wa Sai mjini Mbeya kuelekea makaburini kwa mazishi yaliyofanyika jana kwenye makaburi ya Isyesye.Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

  • Kuhusu uchunguzi huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema baada ya kupata taarifa hizo, kikosi kazi kilifanya kazi usiku na mchana kumsaka na hatua ya kwanza kilipata mawasiliano ya mtekaji na baadaye kubaini kuwa Iringa.

Mbeya. Polisi mkoani Mbeya inamshikilia mtu mmoja kwa madai ya kumteka mtoto Junior Siame (8) na kisha kumnyonga baada ya wazazi wake kushindwa ‘kumkomboa’ kwa Sh10 milioni.

Mtoto huyo, mkazi wa Sai, Mbeya alitekwa na watu wasiojulikana alipokuwa akienda shuleni kwa ajili ya masomo ya jioni (tuition) Aprili 9 na mwili wake ulipatikana juzi mchana katika eneo la Mlima Nyoka baada ya mtuhumiwa ambaye hajatajwa kutiwa mbaroni na polisi na kisha kuwaonyesha mahali alipomtupa baada ya mauaji.

Bakari Siame ambaye ni baba wa mtoto huyo aliyekuwa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Hayanga, alisema Jumanne iliyopita mwanaye alikwenda shuleni na mchana wa saa tisa alirejea nyumbani kama kawaida.

Alisema saa 10 jioni alikwenda kwenye masomo ya jioni na walisubiri hadi jioni muda ambao huwa anarudi nyumbani lakini hakuonekana hivyo kupata hofu. Alisema ilipofika saa moja kasoro jioni, walikwenda kumuulizia kwa rafiki yake ambaye alisema hajamuona, hivyo wakaenda kutoa taarifa kituo cha polisi.

“Jirani yetu fundi friji alikuja hapa na alikuwa akiwasiliana na mtekaji. Huyo mtekaji akatuambia kwa simu kwamba mwanangu anaye huko na anahitaji Sh10 milioni taslimu ndiyo amuachie,” alisema Bakari.

Alisema baada ya kuzungumza na mtekaji huyo alitoa taarifa Polisi na akaambiwa wanaendelea kufanya uchunguzi wa kumnasa.

Kuhusu uchunguzi huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema baada ya kupata taarifa hizo, kikosi kazi kilifanya kazi usiku na mchana kumsaka na hatua ya kwanza kilipata mawasiliano ya mtekaji na baadaye kubaini kuwa Iringa.

“Kikosi kilienda Iringa, tukafanikiwa kumpata mtuhumiwa maeneo ya Ipogolo akiwa amejificha na alipokamatwa alieleza kuwa ndiye aliyeshiriki kwenye tukio la kumteka mtoto Junior na alikwenda jijini Mbeya akaonyesha mahali alipomuulia ambalo ni eneo la Mlima Nyoka karibu na mashamba ya mahindi,” alidai Kamanda Matei.

Alisema baada ya kumhoji, alieleza namna alivyofanikisha kumteka mtoto huyo na kwamba, siku ya tukio alikutana naye barabarani ambako alimuuliza jina lake na anakoishi.

Kamanda Matei alisema mtuhumiwa huyo alieleza kuwa alimuuliza mtoto huyo mali walizonazo nyumbani kwao na kuambiwa kuwa wana nyumba na gari la baba yake ambalo walikuwa na mpango wa kuliuza.

“Alimwambia mtoto huyo waende nyumbani (kwa wazazi wa Junior) wakalione hilo gari, lakini pia akabadilishe nguo za shule, ili wakamtafute mteja wa kulinunua gari la baba yake na mtoto alikubali, wakarudi hadi Sai nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo.

“Lakini hapo nyumbani Sai, pembeni yake (jirani) kuna mtu mmoja ni fundi friji alikuwa ameandika jina na namba yake ya simu na kampuni yake ya kutengeneza friji, mtuhumiwa anasema alinakili namba hiyo akiwa na lengo la kufanya mawasiliano ya kuwapata wazazi wa Junior.

“Hiyo inaonyesha alikuwa na mawazo kwamba atamteka yule mtoto, hivyo mawasiliano ya wazazi wa yule mtoto atayapata kupitia kwa namba ya mtu wa friji na kweli marehemu alifika nyumbani akabadilisha nguo, akavaa track suti nyeusi na viatu vya kuchomeka wakaondoka na mtuhumiwa huyo uelekeo wa Stendi ya Mabasi ya Nane Nane kwa mguu.

“Walipofika stendi walipanda daladala zinazokwenda Uyole hadi Nsalaga na walipofika Nsalaga waliteremka na hapo mtuhumiwa aliendelea kufanya mawasiliano na fundi friji.

“Mtuhumiwa huyu alimueleza fundi aende kwa wazazi wa Junior akisema kuna friji la kutengeneza hapo. Alipofika pale alizungumza na wazazi hao kupitia simu ya fundi friji kwamba yupo naye amemteka na anahitaji apewe Sh10 milioni,” alidai Kamanda Matei.

Alisema baada ya hapo, mtoto Junior alipoona mazungumzo yakiendelea kati ya wazazi wake na mtu huyo aliyekuwa naye (mtuhumiwa) aliona yupo kwenye mazingira ambayo sio ya kwenda kutafuta mteja wa kununua gari bali ametekwa.

Mtoto huyo alianza kulia na kuona hivyo, mtuhumiwa aliamua kumchukua na kumpeleka shambani ili asiendelee kupiga kelele na watu wakamuona.

Alisema, “alipofika kule shambani, mtuhumiwa huyo alimziba mdomo na pua na akawa amemuua mtoto huyo na kumuacha maeneo ya Mlima Nyoka hatua chache kutoka kwenye shamba la mahindi.”

Kamanda Matei alisema walipozidi kumhoji mtuhumiwa huyo, alidai kwamba alipokuwa mfungwa Katika Gereza la Butimba, Mwanza alijifunza mbinu za kupata fedha kwa kuteka mtoto na kwenda kumwambia mzazi wake atoe fedha na ndicho alichokifanya katika tukio hilo.

Alisema mtuhumiwa huyo alifungwa Butimba kwa kosa la kubaka na alihukumiwa kifungo cha miaka 30 lakini alitoka gerezani Februari mwaka huu baada ya kuachiwa kwa rufaa.

Marehemu Junior alizikwa jana katika mazishi yaliyofanyika kwenye makaburi ya Isyesye jijini Mbeya.