Askofu Shoo aponda viongozi wa dini wanaotoa mafundisho potofu

Muktasari:

  • Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fredrick Shoo ameisihi Serikali kuwa makini na manabii na viongozi wa dini wanaotoa mafundisho potofu na kutumia mahangaiko ya waumini wao ili kujitajirisha.

Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fredrick Shoo ameisihi Serikali kuwa makini na manabii na viongozi wa dini wanaotoa mafundisho potofu na kutumia mahangaiko ya waumini wao ili kujitajirisha.

Askofu huyo ametoa kauli hiyo alipozungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu hivi karibuni.

“Ni lazima Serikali ijue historia ya hao (manabii) wanaoibuka na umiliki wa huduma zao uchunguzwe vizuri. Nafikiri Serikali yetu inalo la kujifunza kwa Serikali ya Rwanda,” alisema Askofu Shoo.

Askofu Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, amesema kanisa la kweli limepewa wajibu wa kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili na si kujitajirisha kwa mali na fedha.

Mhadhiri wa vyuo mbalimbali vya dini, Dominic Tarimo alidai wengi wa wachungaji wa madhehebu yanayoibuka kila uchao hawana elimu ya theolojia ya kuwasaidia kuyaongoza.

“Kwa kweli kwa hali tuliyonayo sasa Serikali inatakiwa iweke sheria kali kama ilivyo Rwanda ili kulikomboa taifa hili. Wengine wanajidai wameoteshwa kumbe lengo lao ni sadaka,” amedai Tarimo.

Mkazi wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Tryphone Kamugisha, amesema kila kukicha inakuwa ni afadhali ya jana kutokana na jamii kushuhudia vituko na mafundisho ya ajabu ajabu ya dini.

“Kila kukicha kumekuwa na matukio ya kusikitisha na wengine wanafanya uponyaji kwa kumwagia watu soda, kweli jamani? Yaani tunapokwenda manabii wanakuwa hatari kuliko wanasiasa.”

Kilichofanywa na Rwanda

Machi mwaka jana, Rais Paul Kagame aliagiza kufungwa kwa makanisa zaidi ya 700, ambayo yalidaiwa kutofuata taratibu za ujenzi na kuweka vipaza sauti vya sauti za juu na kuchafua mazingira.

Ilielezwa kuwa baadhi ya makanisa yalikuwa na hali mbaya na mengine yamejengwa na kuezekwa kwa nailoni, mazingira ambayo yapo pia Tanzania kwa makanisa kujengwa kwa maboksi na makuti.

Mbali na kuyafunga makanisa hayo, Rwanda imewataka wachungaji wote wanaotaka kuhubiri injili, kuhakikisha wana shahada ya kwanza ya Thiolojia itakayowasaidia kutoa mafundisho sahihi.

Maafa ya dini duniani

Wananchi mbalimbali wanaonya kuwa endapo mambo ya mafundisho ya dini yataachwa kuwa shaghalabaghala, nchi inaweza kukumbwa na maafa ya kidini kama yaliyotokea Guyana na Uganda.

Novemba 18, 1978 wafuasi 918 wa mchungaji Jim Jones wa Guyana Amerika ya Kusini walikufa kwa kunywa sumu katika “maafa ya kiimani” baada ya kupewa mafundisho mabaya na mchungaji Jones.

Jones hakuwahi kupata mafundisho rasmi ya dini bali aliunganisha falsafa ya dini na ile ya Ujamaa na kufanikiwa kuwashawishi waumini wake kunywa sumu kwa kile alichoita “Revolutionary Suicide”.

Kutokana na ulegevu wa mamlaka za Dola na kutochukua hatua mapema, mwaka 2000 wafuasi wa Askofu Joseph Kibwetere zaidi ya 1,000 nao waliangamia kwa moto nchini Uganda.

Kibwetere aliyewahi kuugua maradhi ya akili mwaka 1980, alidai kupata maono na kumsikia Yesu akizungumza na Bikira Mariam juu ya kusikitishwa na wanadamu wasivyofuata amri 10 za Mungu.

Machi 15, 2000 ikiwa ni siku mbili kabla ya maafa ya waumini wake, Kibwetere alituma barua kwa Serikali ya Uganda akiaga kwamba kizazi cha sasa kimefikia mwisho na mwisho wa dunia umefika.

Kama kawaida Serikali ya Uganda haikushtushwa na barua hiyo na matokeo yake waumini zaidi ya 1,000 waliokusanyika wakisubiri mwisho wa dunia, walichomwa kwa moto ndani ya kanisa hilo.