Assange Kutoka mkimbizi mpaka mgeni asiyetakiwa

Mmoja wa waanzilishi wa mtandao wa Wikileaks, Julian Assange ametiwa mbaroni baada ya kujificha katika ubalozi wa Ecuador nchini Uingereza kwa takribani miaka saba.

Picha na video mtandaoni zinamwonyesha Assange akiburuzwa kuondolewa katika ubalozi wa nchi hiyo uliomhifadhi tangu mwaka 2012, akikimbia kushtakiwa kwa makosa mbalimbali katika nchi za Marekani na Sweden.

Hakupanga kuweka makazi katika ubalozi mdogo huo kwa kipindi kirefu hivyo, lakini kwa bahati alijikuta akipewa hifadhi ya muda mrefu katika chumba cha ofisi kilichogeuzwa cha kulala.

Assange aliomba hifadhi katika ubalozi huo akikimbia kurudishwa Sweden alipokuwa na kesi ya ubakaji akidai kuwa amebambikiwa baada ya kuvujisha siri za mataifa mbalimbali ikiwamo Marekani. Hata hivyo kesi hiyo ilifutwa.

Haikuwa miaka saba iliyojaa amani katika eneo hilo. Mwenyeji na mgeni wake walikuwa katika mvutano. Mwenyeji alitaka mgeni abadilike aache na udukuzi. Mgeni alimtuhumu mwenyeji kutaka taarifa kutoka kwake.

Majuzi, kama mgeni aliyechokwa au asiyetakiwa, alisukwa sukwa na askari wakati akiondolewa katika ubalozi huo uliotumia zaidi ya dola za Marekani milioni moja kwa mwaka kumhifadhi.

Aliondolewa kwa kuviziwa ili asiweze kurudi nyuma japo hatua moja, kwa kuwa aliwahi kumtisha balozi Jaime Merchan kwamba angeweza kubonyeza kitufe ambacho kingeleta madhara makubwa kwa ubalozi.

“Tumemuondoa mtu mtukutu katika himaya yetu, kuanzia sasa tutakuwa makini na watu tunaowapa hifadhi sio kama huyu ambaye nia yake ni ovu ya kutikisa serikali za watu,” alisema Rais wa Ecuador, Lenin Moreno muda mfupi baada ya Assange kuondolewa.

Hata hivyo, Rais wa zamani wa Ecuador, Rafael Correa aliyekuwapo madarakani wakati Assange akipewa hifadhi, amesema hata kama amekosea siyo sahihi kumtupa ‘mdomoni mwa simba.’

Assange inadaiwa alimchokoza Rais Moreno kwa kuchapisha picha zake akiwa amelala kitandani na nyingine za familia yake zikiwa katika sherehe.

Pia, katika mtandao huo alichapisha taarifa kuhusu akaunti za fedha za mdogo wa Rais zilizopo katika nchi mbalimbali.

Taarifa zinasema ni kama mgeni ambaye alichoka kuishi katika nyumba hiyo ndiyo maana aliendeleza vituko kila kukicha.

Anakwenda wapi?

Uingereza itaamua kumsafirisha mpaka Marekani kujibu kesi ya kuvujisha siri za Serikali kupitia mtandao wake wa Wikileaks. Pia, inaweza kuamua kumrudisha kwao Sweden.

Kama akipelekwa Marekani iwapo atapatikana na hatia ya kuvujisha siri kwa kuingilia mawasiliano ya kompyuta, anaweza kuhukumiwa kifungo kisichopungua miaka mitano.

Wakili wake, Jennifer Robinson amesema atapambana mteja wake asipelekwe Marekani kwa sababu anaweza kuhukumiwa kwa kuvujisha taarifa ambazo ilikuwa sahihi kuitaarifu jamii na siyo nyaraka za siri kama inavyoelezwa.

Amesema amemtembelea mteja wake katika vyumba vya mahabusu na amempa ujumbe kwa watu wanaomuunga mkono kuwa anawashukuru sana.

Kwa nini Marekani inatamka Assange?

Mwaka 2006 alianzisha mtandao wa Wikileaks kwa ajili ya kuchapisha taarifa za siri na picha kuhusu watu, taasisi na serikali mbalimbali duniani.

Miaka minne baadaye, mtandao huo uligonga vichwa vya habari baada ya kuchapisha video ikimuonyesha askari wa Marekani akiua raia kutoka juu ya helkopta nchini Iraq.

Hapa ndipo mgogoro kati yake na Marekani ulipoanzia. Aliendelea kuchapisha taarifa mbalimbali za siri za Marekani na mataifa mengine.

Mchambuzi wa masuala ya usalama wa Marekani, Chelsea Manning alikamatwa akihusishwa na uvujaji wa nyaraka za siri zaidi ya 700,000 akishirikiana na Assange.

Sinema ya kumtoa ilianzaje?

Askari wa Scotland Yard wamesema walialikwa na balozi wa Ecuador kumchukua baada ya kujitoa katika kumpa hifadhi wakisema wamefikia kikomo.

Rais wa nchi hiyo, Lenin Moreno alisema: “Imetosha. Nchi yetu imefikia kikomo katika kumsaidia Bwana Assange.”

Moreno amesema: “Ni hivi karibuni yaani Januari mwaka huu mtandao wa Wikileaks ulivujisha taarifa za siri za Vatican. Hii imetuthibitishia kwamba Assange bado anajihusisha na uvujishaji wa siri za mataifa mengine.”

Pia, amesema alikuwa mkorofi ubalozini hapo akitaka aondolewe kamera za CCTV na pia, kukwaruzana na walinzi mara kwa mara.

Hivi karibuni, mtandao wa Wikileaks ulitoa taarifa kwamba umegundua mkakati wa kumchunguza Assange akiwa ndani ya ubalozi huo.

Amekiri kwamba kwa muda mrefu kumekuwa na kutokuelewana katika Assange na ubalozi wa Ecuador ambao ulikuwa ukimkataza kufanya baadhi ya vitu ikiwamo udukuzi.

Hata hivyo, Moreno alisema serikali ya Uingereza ilimhakikishia kuwa Assange hatapelekwa Marekani.

Trump achomoa ishu ya Assange

Rais wa Marekani, Donald Trump amewahi kunukuliwa akisema anaupenda mtandao wa Wikileaks lakini juzi alipoulizwa kuhusu kinachoendelea alisema hafahamu chochote.

“Sifahamu chochote kuhusu Wikileaks, nimekuwa nikiona kuna kitu kinaendelea kikimuhusisha Julian Assange lakini sielewi, hayo siyo mambo yangu,” aliwaambia wanahabari katika mkutano wake na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in.

Mtandao wa CNN unaripoti kuwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni mwaka 2016, Trump alisema anaupenda mtandao wa Wikileaks.