Baba azungumzia siku 40 tangu kutekwa kwa mwanaye Dar

Muktasari:

  • Uchungu wa kuishi siku 40 bila ya kumuona mtoto wake Idrissa Ally (13) unaendelea kumtesa baba mzazi wa mtoto huyo Ally Idd ambaye ameamua kuviachia vyombo vya dola viendelee na uchunguzi wa suala hilo.

Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza uchungu utakaokuwa nao kwa siku 40 iwapo hutajua alipo mwanao? Ndivyo ilivyo kwa Ally Idd, baba wa Idrissa Ally (13) aliyetekwa Septemba 26 kwa staili ya kimafia.

Idd anasema kwa sasa hawezi kuzungumza suala la mwanaye, badala yake anaviachia vyombo vya dola viendelee na taratibu za kumtafuta.

Idrissa, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Princes Gate hadi jana ametimiza siku 40 tangu alipotekwa Septemba 26, saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti wilayani Kinondoni.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva mwanamume aliyekuwa na gari aina ya Toyota IST, ambaye baada ya kuwafukuza marafiki wa Idrissa alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo kisha kumuingiza katika gari lake kupitia mlango wa nyuma.

Idd mwenye watoto wawili wa kiume, Idrissa na Ishac, alisema jana bado vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, hivyo ni vyema akapumzika kuzungumza mara kwa mara wakati linafanyiwa kazi.

“Nikiendelea kuzungumza jambo hili wakati uchunguzi unaendelea siyo sahihi. Acha vyombo vya dola vifanye kazi yake kwa wakati huu, muda ukifika nitazungumza, lakini kwa sasa acha tupumzike,” alisema.

Mwezi uliopita kwa nyakati tofauti Idd alisema nguvu na hamasa kubwa iliyotumika kumsaka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji aliyetekwa kisha kupatikana ihamishiwe kwa watu wengine akiwamo mwanaye.

Alisema, “binadamu wote ni sawa na bado tunaliamini jeshi letu kwa kazi linayofanya lakini litusaidie na sisi, ni muda sasa mwanangu sijamuona.”

Mzazi huyo alisema wanaendelea na maombi kwa Mungu ili mwanaye arejee akiwa mzima, huku akiwaomba Watanzania kutoa taarifa polisi watakapopata taarifa au kumuona Idrissa.

Mwalimu na mama

Mwalimu Mkuu wa Princes Gate, Mussa Idrissa alisema wanafunzi wenzake na Idrissa walikuwa na matumaini kuwa atarudi na kujiunga nao, lakini kadri muda unavyokwenda wanavunjika moyo. “Nikiwa ofisini kwa nyakati tofauti wanakuja na kuniuliza vipi Mwalimu, Idrissa anarudi lini? Wananieleza walidhani kupotea kwake ni jambo la wiki moja au mbili kisha ataonekana, lakini ni mwezi sasa umetimia. Ninawajibu kuwa wasikate tamaa na wazidi kumuomba Mungu, ipo siku rafiki yao atarudi,” alisema Mussa.

Mama wa mtoto huyo, Leila Kombe aliliambia Mwananchi kuwa polisi wamewahakikishia kuwa upelelezi unaendelea.

Oktoba 19, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro alisema kuna dhana iliyopo kuwa kila mtoto akipotea kanisani au kutoonekana nyumbani kwa wiki mbili ametekwa .

“Kutekwa kuna sababu zake, nguvu au silaha imetumika. Sasa mtu anaweza kupotea au baba akiona mtoto wake amemaliza wiki mbili au tatu anasema ametekwa,” alisema Sirro baada ya kuulizwa na wanahabari.

Waziri Lugola

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema Serikali inafuatilia matukio hayo na kwamba licha ya kutokea kwa utekaji huo, watu wamekuwa wakipatikana.

Lugola alisema mwaka 2017, watu 27 walitekwa, polisi iliwapata 22 wakiwa hai, wawili walikuwa wamekufa na watatu hawakupatikana.

“Katika kipindi cha Januari hadi Oktoba 11, 2018 watu 21 walitekwa. Kati yao 17 walipatikana wakiwa hai na wanne hawakupatikana hadi sasa. Watuhumiwa 10 walikamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema Lugola.