Bageni kuhitimisha kesi ya akina Zombe leo

Muktasari:

  • Mahakama ya Rufani leo Jumatano Agosti 14, 2019 inahitimisha kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini wa Mahenge mkoani Morogoro iliyokuwa ikiwakabili maofisa 13 kwa Jeshi la Polisi  kwa kutoa uamuzi wa mwisho kwa ofisa mmoja aliyesalia katika kesi hiyo

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani leo Jumatano Agosti 14, 2019 inahitimisha kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini wa Mahenge mkoani Morogoro iliyokuwa ikiwakabili maofisa 13 kwa Jeshi la Polisi  kwa kutoa uamuzi wa mwisho kwa ofisa mmoja aliyesalia katika kesi hiyo.

Mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi wake kuhusu  maombi ya marejeo ya aliyekuwa mkuu upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni, mrakibu wa Polisi, Christopher Bageni aliyehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya wafanyabiashara hao.

Uamuzi huo ndio unatoa nafasi ya mwisho kwa Bageni, kunusurika katika adhabu hiyo ya kitanzi  au kugonga ukuta kwa kuwa uamuzi wowote utakaotolewa ndio utakuwa wa mwisho.

Uamuzi huo ndio unahitimisha kesi hiyo mahakamani baada ya kudumu kwa miaka 13 tangu washtakiwa walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwaka 2006, huku ikipitia hatua mbalimbali na washtakiwa wakipungua katika kila hatua, hadi kubakia Bageni pekee.

Hata hivyo,  jambo kubwa linalosubiriwa kwa hamu na makundi mawili tofauti ni kujua hatima yake, iwapo uamuzi wa mahakama utabakia kama ulivyo au utabadilika.

Hayo yote yatabainika leo mchana wakati hukumu hiyo itakaposomwa na naibu msajili mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu kuanzia saa nane mchana.

Bageni alihukumiwa na mahakama hiyo adhabu hiyo Septemba 11, 2016 baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara hao watatu wa madini na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam, aliyekuwa akiwaendesha walipokuja jijini kuuza madini yao.

Wafanyabiashara hao wa madini,  Sabinus Chigumbi (Jongo) na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na mwenzao Mathias Lunkombe pamoja na dereva teksi Juma Ndugu.

Waliuawa kwa kupigwa risasi katika msitu wa Pande wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Januari 14, 2006.

Hukumu hiyo iliyomtia hatiani Bageni ilitolewa na jopo la majaji watatu, Bernard Luanda, Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage, kufuatia rufaa aliyoikata Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru, yeye na wenzake wanane.

Wenzake watatu waliokuwa wamesalia baada ya DPP kuwaondoa wengine wanne siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, wao waliponyoka katika adhabu hiyo, baada ua mahakama hiyo kuwaona kuwa hawakuwa na hatia.

Walioponyoka ni aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), kamishna msaidizi wa polisi  (ACP), Abdallah Zombe, aliyekuwa mkuu wa upelelezi, Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Ahmed Makelle, na askari wa kituo cha Polisi Oysterbay, Rajabu Bakari.

Bageni kupitia wakili wake Gaudiosus Ishengoma alirejea tena mahakamani hapo na kufungua maombi ya marejeo akipinga hukumu hiyo, kuomba mahakama iirejee na iitengue, akidai kuwa ina makosa ya dhahiri.

Maombi hayo ya marejeo namba 63 ya 2016, yalisikilizwa Juni 14, 2019 na jopo la majaji watatu, Stella Mugasha, Ferdinand Wambali na Rehema Kerefu.

Ishengoma, katika sababu zake za marejeo pamoja na mambo mengine aliieleza mahakama kuwa hukumu hiyo iliyomtia hatiani mteja wake ina dosari kwani ilimtia hatiani kwa ushahidi ambao hauko kwenye kumbukumbu za mahakama, yaani katika mwenendo wa kesi ya msingi.

Pia alidai kuwa mteja wake hakupewa nafasi sawa ya kusikilizwa kwani hoja ambazo mahakama ilizitumia kumtia hatiani ni mpya  hazikujadiliwa hata kwenye usikilizwaji wa rufaa hiyo.