VIDEO: Batuli kumburuza Mwijaku mahakamani

Wednesday July 3 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msanii wa filamu nchini Tanzania, Yobnesh Yusuf maarufu Batuli ameeleza mpango wake wa kumburuza mahakamani msanii mwenzake, Mwemba Batoni maarufu Mwijaku kwa madai kuwa amekuwa akimchafua kwenye mitandao ya kijamii.

Batuli ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 3, 2019 katika mahojiano na Mwananchi baada ya Mwijaku anayetesa katika tamthilia ya Mahaba kudai mwenzake huyo anatumia tasnia hiyo kama mgongo wa kufanya  mambo yasiyofaa katika jamii ikiwa ni pamoja na kusaka wanaume na hana ushahidi wowote.

Vita ya wawili hao imeshika kasi katika mitandao ya kijamii baada ya Batuli kudai Mwijaku anatafuta kiki kupitia jina lake.

Wakati Mwijaku akilieleza Mwananchi kuwa Batuli hajui kuigiza na kusisitiza kauli yake inayolalamikiwa na mwenzake, Batuli amesema si mara ya kwanza kuchafuliwa na Mwijaku.

Mwijaku alipoelezwa kuhusu kusudio la Batuli kwenda mahakamani alijibu kwa kifupi, “poa”.

Siku za hivi karibuni Mwijaku amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kukosoa mambo mbalimbali yanayofanywa na wasanii kwa madai kuwa anawarekebisha tabia ili warejee kwenye mstari.

Advertisement

Advertisement