Bei ya kunyoa nywele wasichana Sh275,000

Muktasari:

Ripoti ya gharama za maisha katika miji mikubwa 133 iliyotayarishwa na gazeti la Economist inaonyesha Jiji la Paris limekuwa ghali hadi kufikia nafasi ya kwanza pamoja na Singapore na Hong Kong.

 


AFP. Kama msichana anayekwenda Paris nchini Ufaransa akitegemea kushughulikia nywele zake katika jiji hilo la barani Ulaya, itabidi afanye utafiti kabla ya kuamua.

Staili nyepesi ya kunyoa nywele kwa msichana imefikia Sh275,000 kwa mujibu wa ripoti mpya ya gharama za maisha katika miji mikubwa iliyofanywa na Economist Intelligence Unit (EIU) na ripoti yake kutoka leo.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa jiji hilo la Paris limeungana na Singapore na Hong Kong kileleni mwa orodha ya miji ambayo ni ghali kuishi, wakati Venezuela ndiyo nchi ambayo maisha yako chini.

Jiji hilo la Ufaransa ndilo pekee kutoka kanda ya Ulaya kuingia katika orodha ya miji kumi ghali duniani, ikiwa imepanda kutoka nafasi ya pili iliyokuwa inashikilia katika orodha ya mwaka jana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, suti ya kawaida ya vipande viwili kwa mwanaume, yaani koti na suruali pekee, ni Sh4.6 milioni.

Jiji la Paris lina watu milioni 2.14 na tangu karne ya 17 limekuwa ni kitovu cha biashara, taasisi za fedha, fasheni, sayansi na sanaa na linajulikana kutokana na kuwa na majengo mengi ya makumbusho kama Louvre, Musée d'Orsay, Musée de l'Orangerie , kanisa kuu la Notre Dame de Paris, Sainte-Chapelle na mnara maarufu wa Eiffel Tower uliojengwa mwaka 1889.

Mwaka juzi jiji hilo lilitembelewa na watalii milioni 23 na kushika nafasi ya tatu kati ya miji iliyotembelea na watu wengi, likiwa nyuma ya Bangkok na London.

Kupanda kwa thamani ya fedha, kupanda kwa bei za bidhaa na kushuka kwa thamani ya fedha kulichukua nafasi kubwa katika ripoti hiyo ya mwaka huu ambayo iliangazia miji mikubwa 133 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Ripoti hiyo ililinganisha bei 400 za bidhaa na huduma 160, ikiwa ni pamoja na chakula, nguo, pango la nyumba, usafiri, ada na michezo.

Utafiti huo unalenga kuziwezesha kampuni kuchakata malipo ya fidia kwa wafanyakazi wake wataalamu wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.

EIU imesema katika taarifa yake kuwa hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka thelathini kwa miji mitatu kugongana kileleni mwa orodha hiyo, baada ya Singapore lkuongoza chati hiyo mwaka jana.

Orodha hiyo imetawaliwa na miji ya Asia na Ulaya, huku Osaka na Seoul ikishika nafasi ya tano na saba. Nyingine katika nafasi ya tano ni Geneva, wakati Copenhagen pia inashika nafasi ya saba sawa na Seoul. Zurich ni ya nne.

Bara la Amerika Kaskazini limewakilishwa na New York, ambayo pia inashika nafasi ya saba na Los Angeles, ambayo imeshika nafasi ya kumi pamoja na Tel Aviv. AFP