Bendera za ACT zapepea Makao Makuu CUF Z’bar

Muktasari:

Iililokua jengo la makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) Mtendeni mjini Unguja visiwani Zanzibar asubuhi ya leo Jumanne limeanza kupepea rasmi bendera mpya ya chama cha ACT- Wazalendo

Unguja. Siku moja baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza rasmi kujiunga na Chama cha ACT- Wazalendo, iliyokuwa makao makuu ya CUF Mtendeni mjini Unguja visiwani Zanzibar imeanza kupepea bendera ya ACT- Wazalendo.

Uwepo wa hali hii umeibua maswali kwa baadhi ya wananchi na kujiuliza iwapo jengo hili lilikua mali ya chama au ya mtu binafsi.

Baadhi ya wanachama wa CUF kisiwani hapa wakizungumza na Mwananchi walisema hawafahamu kuhusu jengo hilo.

Majda Awadhi amesema anachokifahamu yeye hapo ni makao makuu ya chama na walikua wakiingia na kutoka tu.

“Inawezekana ilikuwa mali ya chama au pia inawezekana walikuwa wanakodi pia, yote ni sawa tu” amesema.

Naye Said Hassan amesema kinachoonekana sasa ni matukio mazuri zaidi kwao kuliko kubaki kwenye mgogoro aliodai hauna tija kwao.

Amesema anaamini hali hiyo viongozi wanaifahamu na watakua wamejipanga vyema kutetea iliyokuwa makao makuu ya chama hicho iwapo upande wa Profesa Ibrahim Lipumba utadai ni sehemu ya mali ya chama.

Alipoulizwa na Mwananchi aliyekua Mkurugenzi wa habari wa chama cha CUF, Salim Bimani upande wa Maalim Seif, amesema kwa sasa si suala la kujadili na muda ukifika kila kitu kitajulikana ukweli wake.

Amesema kwa sasa wananchi wafahamu kuwa iliyokua jengo la makao makuu ya CUF imegeuka rasmi kuwa ofisi ya ACT- Wazalendo Zanzibar.