Biashara mpya kusamehewa kodi kwa miezi 6 awali

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phili Mpango 

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imependekeza kusamehe kodi mfanyabiashara au mwekezaji kwa kipindi cha miezi sita pindi anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imependekeza kusamehe kodi mfanyabiashara au mwekezaji kwa kipindi cha miezi sita pindi anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

Msamaha huo, utaanza kutumika Julai Mosi 2019, ili kumuwezesha mfanyabiashara au mwekezaji kujiandaa na mahitaji yanayotakiwa katika shughuli anazofanya.

Vile vile kuondoa usumbufu, dhana ya woga wakati wa kuanza biashara ikiwamo mahitaji ya leseni ya biashara na vibali vingine.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 13, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phili Mpango wakati akiwasilisha makadirio na mapato ya Serikali kwa mwaka 2019/20.

Waziri Mpango amesema, “Hatua hii inatofautiana na hali ilivyo sasa ambapo mfanyabiashara anapopewa TIN anaanza kufanyiwa tathimi (tax assessment) ya mapato yake ya biashara na kutakiwa kulipa kodi.”