BoT: Tutaendelea kuchukua hatua maduka ya fedha

Muktasari:

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka watu kutumia huduma rasmi za ubadilishaji fedha na kuripoti wanapopata usumbufu


Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaendelea kuchukua hatua kwa watoa huduma na watumiaji wa huduma za ubadilishaji fedha zisizo rasmi kwa sababu ni kinyume na sheria.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni siku chache tangu kufanyika kwa operesheni maalumu ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni Novemba 2018 jijini Arusha na kufungia baadhi ya maduka bubu ambayo hayana leseni yaliyokuwa yanaeendesha huduma hiyo kinyume na sheria.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Januari 31, 2019 imezitaka taasisi za fedha kuendelea kutoa huduma ya ubadilishaji fedha kwa watu wote wakati uchunguzi wa maduka bubu yaliyofungwa Arusha ukiendelea.

“Tunautahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi za ubadilishaji fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali zinazotokana na huduma hizo ikiwamo kuibiwa na kupewa fedha bandia,” taarifa inaeleza.

Pia, wananchi watakaopata usumbufu wowote wakati wa kubadilisha fedha za kigeni wanatakiwa kutoa taarifa ili wapatiwe ufumbuzi.

 “Huduma za ubadilishaji fedha kwa sasa zinapatikana katika benki na taasisi za fedha zinazoendesha biashara nchi nzima na tunazihimiza benki hizi kuendelea kutoa huduma kwa watu wote,” taarifa inaeleza.