Bosi Tanroads alezea daraja la Busisi Mwanza itakavyokuwa

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imetiliana saini na kampuni mbili za ujenzi kuanza rasmi ujenzi wa daraja la Busisi-Kigongo, Mwanza nchini Tanzania lenye urefu wa kilomita 3.2 kwa gharama ya Sh582 bilioni.

 

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Patrick Mfugale amesema daraja la Busisi litakalojengwa kwa miezi 48 litakuwa na nguzo 64, ukubwa wake utaruhusu upitaji wa baiskeli, pikipiki na magari ya ukubwa tofauti bila usumbufu na gharama yake itakuwa ni Sh582 bilioni bila VAT.

Mfugale amesema hayo leo Jumatatu Julai 29, 2019 wakati wa utiaji saini wa ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 kutoka Kigongo hadi Busisi likikatiza katika ziwa Victoria.

Kampuni iliyojenga Daraja la Magufuli Kilombero na ile inayojenga barabara za juu katika makutano ya barabara Ubungo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ndizo zilizoshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo.

“Usanifu ulifanywa na kampuni nne, mbili za Kitanzania na mbili za Kikorea … waliochukua vitabu vya zabuni walikuwa 33 lakini waliorudisha walikuwa 11 tu, kampuni zilizoshinda ni hizi mbili na tuna imani na uwezo wake,” amesema Mfugale.

Amesema Tanroads itasimamia vizuri mradi huo ambao utaanza mara moja ili ikiwezekana muda wa kukamilika upungue.