Bosi elimu Dar aeleza utaratibu wa viboko shuleni

Dar es Salaam. Ikiwa ni takriban miezi minane tangu Sperius Eradius (13), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Kagoma wilayani Bukoba afariki dunia kwa kipigo kutoka kwa mwalimu wake, adhabu ya viboko shuleni imeendelea kuumiza vichwa vya wadau wa elimu nchini.

Sperius alifariki kwa kipigo Agosti 27, 2018 kutoka kwa mwalimu wake, Respicius Mtazangira. Machi 6, Mahakama Kuu ilimhukumu mwalimu huyo kunyongwa hadi kufa.

Jana, ofisa elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamisi Lissu alisema adhabu ya viboko haitakiwi kutolewa bila ruhusa ya mwalimu mkuu.

Pia, alisema ruhusa inapotolewa viboko hivyo havitakiwi kutolewa zaidi ya vinne na kwamba, kabla ya adhabu hiyo ni lazima mwanafunzi apimwe afya yake.

Lissu alisema hayo alipokuwa akizungumza katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Ualimu Ebonite kilichopo wilayani Ubungo.

Alisema viboko havijakatazwa, lakini kabla ya adhabu hiyo ni lazima utaratibu ufuatwe.

Ofisa huyo alisema mwongozo huo umekuja baada ya kubaini kuwa wanafunzi wamekuwa wakidhalilishwa huku makosa wanayoadhibiwa nayo yakiwa madogo, lakini wanachapwa viboko sehemu mbalimbali ya miili yao zaidi ya vinne.

“Nawaomba walimu mzingatie hayo, msipofanya hivyo mtajikuta mnaingia kwenye matatizo, inaweza ikatokea mwanafunzi ana matatizo ya kiafya umemchapa akakufia, hiyo inakuwa ni kesi,” alionya Lissu.

Akizungumzia utaratibu, alisema mwalimu mkuu akitoa ruhusa ya adhabu hiyo mwanafunzi wa kike anatakiwa kuchapwa mikononi na wa kiume matakoni na siyo sehemu nyingine ya mili yao.

Pia, aliwataka wamiliki, wakuu wa shule na vyuo kuacha utamaduni wa kuwafukuza wanafunzi bila ya kufuata miongozo iliyowekwa na watakaokwenda kinyume na hilo watachukuliwa hatua za kisheria.

“Mwanafunzi anapofanya kosa kinachotakiwa bodi ya shule au chuo kinakaa kikao ambacho kina maamuzi ya kumfukuza mwanafunzi na siyo mkuu au mmiliki wa shule, na inapotokea kuna tatizo sisi (Idara ya Elimu) tunaibana bodi.”

Mkuu wa chuo, Mwijuma Mirambo aliomba vitabu vya ufundishaji viendane na mitalaa mipya.

“Tunamuomba Rais John Magufuli akutane na wamiliki wa vyuo na shule binafsi tuweze kumpa matatizo yetu yanayotukabili, sasa hivi tuna wakati mgumu, vyuo vingi vimefungwa tunataka tutoe malalamiko yetu,” alisema.

Machi 26, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza kusikitishwa na adhabu kali zinazotolewa kwa wanafunzi, akitoa mfano wa ile iliyosababisha kifo cha Sperius.

Majaliwa alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa sita wa Umoja wa Maofisa wa Elimu na Mikoa (Redeoa) mjini Dodoma.

“Ninatambua si kusudio la walimu kuwadhuru wanafunzi, lakini tukubaliane kuwa kuna udhaifu katika utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni,” alisema Majaliwa.

“Maofisa elimu kawakumbusheni walimu wote nchini wazingatie mwongozo wa kutoa adhabu shuleni chini ya kifungu cha 61 cha Sheria ya Elimu sura 353 pamoja na kanuni zake. Na adhabu hii itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi. Nina hakika tukisimamia utaratibu, matukio haya yaliyoanza kuonekana yatakoma.”