CAG: Neno udhaifu ni la kawaida

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ametoa msimamo kuhusu mzozo kati yake na Spika wa Bunge, Job Ndugai akisema yupo tayari kuhojiwa kama ilivyoelezwa na kiongozi huyo wa mhimili huo wa kutunga sheria baada ya kusema kuwa Bunge ni dhaifu.

“Maneno kama udhaifu au upungufu ni lugha za kawaida kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya mifumo na utendaji katika taasisi mbalimbali. Kama mmewahi kupitia baadhi ya ripoti zangu, mtaona maneno haya yametumika mara nyingi katika kukazia maudhui mbalimbali ya hoja za ukaguzi,” alisema Profesa Assad.

CAG alitoa kauli hiyo jana mchana katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni saa chache baada ya Ndugai kuzungumza na wanahabari na kueleza kuwa katika mabunge ya Jumuiya ya Madola mkaguzi wa hesabu za serikali ni sehemu ya maofisa wa Bunge.

Juzi, Ndugai alizungumza na Mwananchi na kueleza kuhusu uamuzi wa Bunge kutofanya kazi na ofisi ya CAG baada ya Profesa Assad wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kueleza kuwa kushindwa kutekelezwa kwa ripoti anazowasilisha bungeni huenda kunatokana na udhaifu wa chombo hicho, kauli ambayo Ndugai alisema ni ya kudhalilisha Bunge na kumtaka kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Januari 21 kuhojiwa.

Katika mahojiano hayo, Ndugai alisema mzozo wake na Profesa Assad ni wa muda hadi hapo suala hilo litakapomalizika.

Wakati viongozi hao wakieleza hayo, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema jana kuwa wataendelea na harakati za kufungua kesi ya kuomba Mahakama itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.

Wabunge watano wa vyama vitatu vya upinzani, wakiongozwa na Zitto, juzi walikwama kusajili kesi yao baada ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kukataa kwa madai kwamba ina kasoro za kisheria.

Kutokana na uamuzi huo, Zitto na wakili Fatma Karume waliwasilisha malalamiko kwa Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma ambaye baada ya kuyasikiliza, alimwandikia barua Jaji Kiongozi akimwelekeza ashughulikie suala hilo.

Ndugai afafanua

Akizungumza jana na wanahabari baada ya kueleza yaliyojiri katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Chama cha Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika (CPA), Ndugai alisema busara ya kumuita Profesa Assad katika kamati inalenga kuepuka lawama ambazo zinazoweza kujitokeza katika hatua za kinidhamu dhidi yake.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya wanahabari kutaka ufafanuzi kuhusu uhalali wa Ndugai kumhoji CAG,anayelindwa kikatiba kupitia ibara ya 143(6) inayobainisha kuwa CAG hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali isipokuwa mahakama inaweza kutumia madaraka yake kumchunguza CAG.

Alisema, “Yuko rafiki yetu mmoja amekuwa akidanganya kwamba, Spika wa Uganda aliwahi kumwita CAG wa kule halafu sijui ikawaje, niliongea na wabunge wa Uganda wakasema huo ni uongo mkubwa, kule Uganda mfumo wake ni ule wa Madola, ambapo CAG ni ofisa wa Bunge, ndivyo ilivyo huko. Hata Kenya ofisa wa Bunge atamgomea Spika?” alihoji huku akicheka.

“Hawa (CAG) kwa kawaida katika Madola ni maofisa wa bunge, anatoka kwenye mhimili ambao kazi yake ni kusimamia Serikali, sasa badala ya wabunge kwenda kufanya hiyo kazi, wanaajiri mtu anaitwa CAG, anaenda kuchunguza hesabu halafu anawaletea majibu ya alichokiona.

“Hao ndiyo wanaamua kuilekeza, kuishauri Serikali na kadhalika, sasa tangu lini amekuwa bosi wao tena? Kwa hiyo haya mambo yako wazi, tarehe 21 atakuja, asipokuja tutamwonyesha bosi wake ni yupi.”

Ndugai alisema hatua ya Profesa Assad kudhalilisha bunge hilo nje ya nchi ni utovu wa maadili unaoweza kumwajibisha kiongozi yeyote aliyekula kiapo cha maadili.

Akijibu maswali ya wanahabari kuhusu hatua zinazochukuliwa na Zitto, Ndugai alisema mbunge huyo amekuwa akimpa tabu sana pale anapotaka kumuadhibu.

“Eeee.. unajuaa niseme ukweli huyu mbunge amekuwa akinipa tabu sana, ananipa taabu sababu ndiye mbunge mmoja wa chama chake, hawa wengine huwa nafukuza sababu wenzao wapo, sasa huyu (Zitto) ni mmoja tu wa chama chake (ACT Wazalendo),” alisema.

Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari aliyehoji ni kwa nini Bunge lisimchukulie hatua Zitto kama mbunge huyo anapotosha ukweli kuhusu sakata la CAG.