CCM Manyara kuyakata majina ya wenyeviti waliouza ardhi

Muktasari:

Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kata za Simanjiro waagizwa kukata majina ya wenyeviti wa vitongoji na vijiji waliodalalia na kuuza ardhi.

Simanjiro. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara nchini Tanzania, Awadhi Omary amewaagiza wenyeviti wa Kata za wilaya hiyo kutopitisha majina ya wenyeviti wa vitongoji na vijiji waliodalalia na kuuza ardhi ya maeneo yao kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa Oktoba, 2019.

Omary aliyasema hayo jana Jumamosi Agosti 10,2019 mji mdogo wa Terrat kwenye tathimini ya utendaji kazi wa viongozi iliyoandaliwa na Ofisa Tarafa ya Terrat, Lekshon Kiruswa.

Alisema wenyeviti wote wa vijiji na vitongoji ambao wameuza ardhi ya wananchi, wakichukua fomu za kugombea upya wanapaswa kukatwa majina yao kupitia kamati ya siasa ya kata.

"Endapo mtapitisha majina ya viongozi ambao wanajulikana kuwa wameuza ardhi sisi kamati ya siasa ya CCM wilaya na wajumbe wa halmashauri ya wilaya tutakata majina yao kwani watatusumbua kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa," alisema Omary.

Hata hivyo, diwani wa Komolo, Michael Haiyo alisema viongozi wa wilaya wasitumie kigezo hicho kwa kukata majina ya baadhi ya viongozi ambao wanapendwa na wananchi kwa kigezo cha kuwa waliuza ardhi.

"Mfano mimi nilifanyiwa vitimbwi vingi wakati fulani lakini niliangushwa na wapinzani wangu ila nikawaunga mkopo kwenye uchaguzi mara mbili sasa hivi wanasema nimekuwa babu ila nitatoa uamuzi muda ukifika," alisema Haiyo.

Diwani wa Terrat, Jackson Ole Materi alisema anafurahia kikao hicho hakijawatuhumu wao katika uuzaji wa ardhi hivyo wataendeleza mazuri hayo.

"Suala la mgongano na mwenyekiti wa kijiji ni katika kuimarishana tu hakuna tatizo na hadi sasa tumeshikamana pamoja," alisema Ole Materi.