VIDEO: CCM yajihakikishia ushindi chaguzi zijazo, yataja mikoa ya Arusha, Kilimanjaro

Monday June 24 2019

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole akizungumza na waaandishi wa habari katika ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ikiwa imesalia miezi kadhaa kufikia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2019, Chama cha Mapinduzi (CCM) imejihakikishia ushindi wa kishindo kutokana na mtaji mkubwa wa wanachama wake.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema ushindi huo unatarajiwa pia kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Akizungumza leo Jumatatu Juni 24, 2019 katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, Polepole amesema idadi kubwa ya wanachama walionao, miradi mikubwa ya maendeleo, kutetea haki za wanyonge, uboreshaji wa huduma za kijamii na mambo kadha wa kadha yaliyofanywa na Serikali yanawahakikishia kuwa CCM itashinda.

“CCM ina wanachama 15 milioni. Wapiga kura mwaka 2020 wanatarajiwa 21 milioni. Tukisema mwaka 2020 wakapige kura wana CCM pekee kwa wastani wa chini tutapata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 71.”

“Tukisema tufanye kampeni za kawaida kabisa kila wanachama watatu wakatafute mpiga kura mmoja tutakuwa na wapiga kura milioni 20. Hii ina maana ushindi utakuwa wa zaidi ya 90. Kwa maana hii ushindi wa CCM kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu tutashinda kwa kati ya asilimia 71 hadi zaidi ya asilimia 90” amesema Polepole.

Kuhusu kanda ya kaskazini kuwa ngome ya Chadema, Polepole amesema hoja hiyo haina ukweli huku akieleza mikoa ya Arusha na Kilimanjaro iko salama mikononi mwa CCM.

Advertisement

“Wapinzani waliingia Arusha na Kilimanjaro kwa sababu ya tofauti zetu zilizokuwepo ndani ya chama lakini tumeshazimaliza, tumeanza kurudisha himaya yetu na sasa hivi nawaambia 2020 hakuna mpinzani atakayebaki kanda hiyo wameshakwisha,” amesema

Polepole ameongeza kuwa chama hicho hakitowapa nafasi ya kugombea tena viongozi ambao walishindwa kutekeleza majukumu yao na ilani ya chama hicho.

“Viongozi wanaotakiwa na chama hicho ni wale wanaotekeleza maelekezo ya chama ikiwemo uchapakazi, uadilifu, uaminifu, unyenyekevu, wanaochukizwa na rushwa na ubadhilifu wa mali za umma, wazalendo na wakali kwenye mambo ya hovyo,”.

Advertisement