CCM yajipanga kujishusha chini

Friday February 8 2019

Naibu Kaibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla

Naibu Kaibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma Mabodi (katikati) akisaidia kumwaga zege  alipokuwa akishiriki kazi ya ujenzi wa Tawi la CCM lililopo Ng’ambwa Mkoa wa Kusini Unguja, juzi. Na Mpigapicha Maalum 

By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma maarufu Mabodi amewataka viongozi wa CCM kusherekea miaka 42 ya chama hicho kwa kushuka kwa wananchi kusikiliza matatizo yao.

Kauli hiyo aliitoa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji ilani na kushiriki shughuli za jamii, ikiwa ni maadhimisho ya kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa CCM katika mkoa wa Kusini Unguja.

Mabodi alisema CCM ndani ya miaka 42 imepambana na mawimbi na mikwamo ya kisiasa, lakini imefanikiwa kushinda bila kugawanyika hali inayodhihirisha ipo imara.

Alisema kuimarika kwa misingi ya demokrasia, haki za binadamu, utawaka bora na ustawi wa maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii havikupatikana kwa urahisi bali ni zao la sera, miongozo na mipango endelevu ya utendaji inayosimamiwa na CCM.

Alisema makada, wanachama na viongozi wanajivunia kuwa na taasisi inayojali utu na maendeleo ya wananchi wote.

Naye mwakilishi Paje, Jaku Hashim Ayoub alisema ametekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 na kwamba anaendelea kutatua changamoto mbalimbali.

Ziara hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na kufanya shughuli za kijamii, ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Katika ziara hiyo, Dk Mabodi alitembelea maeneo mbalimbali kikiwamo kijiji cha Uchukuni ambako ujenzi wa shule ya msingi; Kisiwa cha Uzi ambako linajengwa tawi la CCM Ng’ambwa; kukagua eneo la daraja lililopendekezwa kujengwa na marehemu Abeid Amani Karume huko Uzi.

Pia, alitembelea tawi la CCM Mungoni na kuweka jiwe la msingi maskani ya CCM Mawe Mawili eneo la Mtule Paje.

Advertisement