CCM yatoa neno Nassari kuvuliwa ubunge, Chadema washtuka

Friday March 15 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Sakata la kuvuliwa ubunge kwa mbunge wa jimbo la Arumeru, Mashariki Joshua Nassari (Chadema) limepokewa kwa hisia tofauti mkoani Arusha, ambapo wakati CCM ikipongeza, Chadema wameeleza kushtushwa na wananchi wanataka ukweli wa jambo hilo uwekwe wazi.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Ijumaa Machi 15, 2019, viongozi wa vyama vya CCM na Chadema, wananchi na viongozi wa Serikali kila upande umeeleza hatua ya Spika kutangaza kuvuliwa ubunge kwa mtazamo tofauti.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe alisema, Nassari amevuna alichopanda kwani alitaka ubunge ili kutekeleza maslahi yake badala ya kuwatumikia wananchi.

"Nassari si bungeni tu hata jimboni haonekani na kilichotokea ni funzo kwa wabunge wote watambue wanachaguliwa kuwatumikia wananchi na si kujali maslahi yao," alisema.

Alisema  wananchi wa Arumeru Mashariki pia wamejifunza wanapochagua wawakilishi wao, wachague watu ambao wana uwezo na si vijana kama Nassari ambaye alikuwa bado anataka kwenda kusoma na kuishi na familia yake.

"Tunampongeza Spika Ndugai kwa uamuzi wake lakini pia ametoa elimu kwa wanaotaka kuwa wabunge lazima wawe wamejiandaa kutetea watu na kama wanaona hawajakamilisha mambo yao binafsi ni bora kutogombea," alisema.

Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Arumeru Mashariki, Gadiel Mwanda licha ya kueleza kusikitishwa na uamuzi wa Spika, aliwataka wananchi wa Arumeru kuwa watulivu kwani suala hilo linashughulikiwa.

"Tunapita katika wakati mgumu sana, tunaomba wananchi wawe watulivu, Nassari alitoa sababu za kutokuwepo bungeni na tunafuatilia jambo hili kwa kushirikiana na viongozi wa kitaifa na wanasheria," alisema.

Hata hivyo, wakati viongozi hao wa kisiasa wakilipokea suala hilo kwa mitazamo ya kisiasa, baadhi ya wakazi wa jimbo la Arumeru Mashariki, wametaka ukweli wa jambo hilo ujulikane na kama mbunge wao amefanya makosa kweli wanaunga mkono Spika.

Jeremiah Kaaya mkazi wa Usa River jimbo la Arumeru Mashariki alisema, uamuzi wa Spika wameupokea kwa sura mbili kwanza, kutaka wabunge wawajibike lakini pia huenda kuna mambo ya kisiasa.

"Mimi sipingani na Spika ila kama ni kweli Nassari hakwenda bungeni bila taarifa adhabu ni sawa lakini kama alitoa taarifa basi tunaomba ukweli ujulikane," alisema.

Elias Pallangyo mkazi wa Kikatiti wilayani Arumeru, alisema Nassari amekuwa kimya kwa muda mrefu hivyo, kama alikuwa na matatizo ya kifamilia alipaswa pia kuwaeleza wananchi na Bunge.

"Ni kweli mbunge wetu amekuwa kimya, tuliambiwa awali anasoma Uingereza lakini baadaye tumesikia kumbe mke wake alikuwa anaumwa sasa, ajitokeze kusema ukweli," alisema.

Ester Minja mkazi wa Tengeru, alitaka vyama vya siasa kuwa na utaratibu wa kuwasimamia wabunge wao, kushiriki vikao vya Bunge na kurejea majimbo ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.

"Mimi bungeni siwaonagi wabunge wengi tu, siku nyingine viti vinabaki tupu sasa vyama vya siasa ndio vimewapeleka hawa wabunge bungeni lazima viwe vikali na kuwachukulia hatua kuliko sasa kuliingiza Taifa hasara ya kufanyika chaguzi za marudio," alisema Minja

Hata hivyo, imebainika kuwa, Nassari licha ya kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge pia katika  vikao vya kamati ya ushauri mkoa wa Arusha (RCC) na kikao cha Barabara mkoa Arusha, mahudhurio yake ni hafifu.

Ofisa habari katika ofisi ya mkoa wa Arusha, Alice Mapunda alisema katika vikao vya mwisho wa mwaka, Mbunge huyo hakuonekana.

Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano, Job Ndugai juzi, ametoa taarifa ya jimbo hilo kuwa wazi kutokana na mbunge huyo, kutoonekana katika vikao vitatu mfululizo vya Bunge na kumtaarifa mkurugenzi Tume ya Uchaguzi kutangaza jimbo hilo kuwa wazi.

Advertisement