CWT yawaonya walimu

Muktasari:

Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), imesema kuna baadhi ya walimu wanasababisha  malalamiko Serikalini kuhusu uhalali wa umiliki wa mali zao.

Dodoma. Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), imewataka walimu wanaopeleka malalamiko yasiyo na tija Serikalini kuacha kufanya hivyo, kwa sababu wameanza kuwachoka baada ya kuchunguza na kugundua hayana ukweli.

Akizungumza jijini hapa leo Jumapili Juni 9, 2019, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Clement Mswanyama amesema mali za chama hicho yakiwamo majengo, Benki ya Mwalimu (MCB) na viwanja zipo kihalali.

Amesema wanachokiona kuhusu taarifa zilizosambaa ni kuna watu wanataka kupotosha kuhusu ukweli huo kuhusu umiliki wa mali za chama hicho kuwa haziko mikononi mwa walimu.

“Walitafuta uongozi lakini walikosa sasa wanatafuta njia zote lakini hawawezi. Tuko stable (imara)  mfumo wa utoaji wa fedha za CWT ni mgumu sasa,” amesema.

Amesema chokochoko za umiliki wa viwanja 29 vilivyonunuliwa Morogoro mwaka 2015 kuwa hazimilikiwi na chama hicho,  zina mikono ya watu ambao wamekuwa wakichochea kwa nia ya kujipatia fedha.

“Tulivyochunguza tulibaini kuna miongoni mwetu walienda kumwambia usikubali  dai fedha (mtu aliyekuwa akivitumia viwanja hivyo kulima). Lakini ukweli ni kwamba alishaandika nyaraka na zipo za kuji-commit kwamba sio eneo lake. Nyaraka hizi zipo mpaka manispaa, Serikali za mitaa,” amesema.

Amesema wanafahamu kuna viongozi wenzao wako nyuma yao na wamekuwa wasaliti kwa nia ya kupata fedha  bila  jasho.

“Sisi hatuwezi kuwachukulia hatua (wanaochochea migogoro) kwa sababu tumebana mianya yote, tumesimama, tunaendelea na mambo yetu,  tunaendelea kuwahudumia wanachama ambao ni walimu,” amesema.

Ameishukuru  Serikali kuwa imeendelea kuwapa ushirikiano na kuwaomba walimu wenzake kuacha kuisumbua Serikali kwa kupeleka malalamiko yasiyo ya tija.

“Chama cha walimu kimesimama vizuri hakuna tatizo ila ni wale watu wenye tatizo na wanataka kuisumbua Serikali. Ningeomba  walimu watulie wachape kazi,  waache kupeleka maneno Serikalini hadi sasa imeanza kuwachoka watu wanaopeleka maneno ambayo hayana tija,” amesema.

Amesema  wao wameshatoa maelezo Serikalini kuhusu malalamiko ya walimu hao na kwa sababu ina vyombo vya uchunguzi wamefanya uchunguzi na kubaini hayana ukweli.