VIDEO: Chadema yazungumzia kupatikana kwa mwanaharakati Mdude

Muktasari:

Chadema yawataka polisi kutochelewa kutoa ripoti juu ya tukio hilo ikisema iwapo watachelewa wao wasilaumiwe

Dar es Salaam. Chadema imelitaka Jeshi la Polisi kueleza kilichomtokea Mdude Nyagali maarufu Mdude Chadema aliyepatikana jana usiku baada ya kutekwa kwa siku tano.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema amesema leo, Mei  9, 2019 kuwa polisi isipotoa taarifa hiyo mapema, Chadema wataeleza.

Mrema amesema kwa sasa hawataki kuingilia kazi ya polisi kwani wanaamini watafanya kwa uadilifu, lakini ni muhimu wakaueleza umma kinachoendelea.

“Wameshamhoji Mdude na tuna taarifa kuwa katika uchunguzi wao kuna watu wengine kule Songwe wamehojiwa, basi waondoe hii taharuki kwa kuweka wazi angalau kidogo kuhusu suala hili,” amesema Mrema.

 

Amesema, “wakishindwa kufanya hivyo kwa haraka, basi sisi hatutanyamaza tutaweka wazi kile ambacho Mdude aliwaambia polisi maana wakati anahojiwa viongozi wa chama walikuwepo.”

 

Kwa mujibu wa Mrema mapema leo asubuhi, maofisa kadhaa wa polisi walifika kwenye hospitali anayotibiwa Mdude na kumhoji licha ya kutokuwa kwenye hali nzuri.

 

Mrema amesema, “haikuwa rahisi kukubali hilo (la kumhoji) lakini tukaona ni afadhali ahojiwe na kueleza anavyokumbuka hata kama ni kwa shida ili polisi wafanye kazi yao.”

 

Mrema ameeleza kuwa Mdude ana majeraha kadhaa na asubuhi ya leo ameingizwa katika chumba cha upasuaji baada ya majibu ya kipimo cha CT scan kutolewa.