DC Machali adaiwa kujihami kwa bastola

Muktasari:

  • Wakati Mkuu wa Wilaya Nanyumbu, Moses Machali akidai kunusurika kukatwa panga akiendesha harakati za kuhamasisha wajasiriamali kuchukua vitambulisho, Polisi mkoani Mtwara imesema aliwatishia bastola wauza madafu baada ya kutofautiana kauli

Dar es Salaam. Wakati Mkuu wa Wilaya Nanyumbu, Moses Machali, akidai kunusurika kukatwa panga akihamasisha wajasiriamali kuchukua vitambulisho,  Polisi mkoani Mtwara imesema aliwatishia bastola wauza madafu baada ya kutofautiana kauli.

Hata hivyo, Mwananchi Digital halikufanikiwa kupata maelezo ya upande wa pili wa kijana huyo anayetuhumiwa.

Katika mitandao ya kijamii leo Jumatatu Aprili 29, 2019 kuna taarifa inayosambaa ikieleza namna Machali alivyonusurika katika tukio hilo baada ya kufika kijiji cha Mikangaula wilayani humo.

Machali alithibitisha taarifa hiyo inayoeleza baada ya kufika kijijini hapo, alisimama kununua madafu huku akikagua wenye vitambulisho na kuhamasisha wasio navyo kulipia lakini mmoja wa wauza madafu alianza kukashifu Serikali akisema inawaibia wananchi.

“Ni kweli ilitokea, nilienda kutoa taarifa jana Kituo cha Polisi cha Mangaka wilayani hapa, kwa hiyo siwezi kuzungumzia kwa kina liko chini ya uchunguzi,” amesema Machali.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Blasius Chatanda, amesema taarifa alizopata kutoka eneo la tukio hilo ni kwamba baada ya kutofautiana kauli na kijana huyo, Machali alitoa bastola kumtishia.

“Niko safari Morogoro. Hata hivyo, taarifa za awali nilizozipata ni kwamba yeye (DC) alimtolea bastola  muuza madafu baada ya kupishana lugha, sasa mazingira ya kutoa hiyo bastola sijui lakini mpigie msaidizi wangu ofisini atakupa taarifa za kina, ”amesema Chatanda.

Akisimulia sakata hilo, Machali amesema katika hali ya kustaajabisha muuza madafu huyo mkazi wa Msufini alianza kutoa maneno ya kashifa Serikali.