DPP atoa saa 48 wapangaji nyumba zilizotaifishwa kuhama

Muktasari:

 

  • Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania, Buswelu Maganga amewataka wapangaji kwenye nyumba za Serikali zilizotaifishwa kuhama kabla ya kuondolewa kwa nguvu pindi wakigoma kuondoka kwa hiari

Mwanza. Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Buswelu Maganga amewapa siku mbili wapangaji sita waliokuwa wanaishi kwenye nyumba za Serikali zilizotaifishwa za Pastory Mayila kuhama kuanzia Januari 22 hadi 25 mwaka huu.

Akizungumza jana maeneo ya Buhongwa jijini Mwanza, Maganga alisema Februari 27 mwaka  2017  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitoa amri ya kutaifisha nyumba sita, magari manne pamoja na eneo la ekari tano lililopo eneo la Buhongwa mali za Pastory Mayila.

“Pastory Mayila alihusika kwenye wizi wa Sh3.7 bilioni na alishirikiana na wenzake kufoji nyaraka kwa kamishna wa TRA na kutumia fedha hizo kujengea na kununua mali hizo zilizotaifishwa na Serikali.”

“Kulikuwa na fedha kutoka TTCL  ambazo zilikuwa zinalipwa TRA kama VAT ambapo yeye kwa kushirikiana na watumishi wa TRA walifanya wizi huo wa kufoji nyaraka za malipo na kulipa kampuni yake ya UEE ambapo Mayila alikuwa muhasibu wa kampuni hiyo,” alisema.

 Maganga alisema Mahakama ilitoa maelekezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha nyumba hizo na magari zinakuwa chini ya Serikali na fedha zinazotokana na wapangaji waliopo zitunzwe lakini tangu mwaka 2017 kipindi hicho  wapangaji hao hawajawahi kulipa fedha yoyote kwa Serikali na bado wanaishi ndani ya nyumba hizo.