Diaspora kutangaza fursa za uwekezaji Tanzania

Muktasari:

Jukwaa hilo linalofanyika Dallas katika jimbo hilo na kujulikana kama Tanzania Day, kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2017.

Dar es Salaam. Huenda Tanzania ikanufaika na uwekezaji kutoka Jimbo la Texas nchini Marekani kutokana na kuwapo jukwaa la kila mwaka linalowakutanisha Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora), viongozi wa Serikali na wafanyabiashara.

Jukwaa hilo linalofanyika Dallas katika jimbo hilo na kujulikana kama Tanzania Day, kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2017.

Katika jukwaa hilo la mwaka 2017, maonyesho mbalimbali ya bidhaa za Kitanzania na mikutano ya kibiashara ilikuwa ni sehemu ya tukio hilo.

Mwaka huu, jukwaa linatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 26 hadi 28.

Mmoja wa waandaaji wake, Ben Kazora (pichani) alisema jukwaa hilo hutumika kuitangaza Tanzania na kuueleza ulimwengu mambo gani wanaweza kufanya kuvutia uwekezaji ambao ni msingi mzuri wa maendeleo ya uchumi.

“Ni Dallas tu, shughuli hii imekuwa ikifanyika, kuna mabilionea zaidi ya 24, pato lake la jumla pengine ni mara 10 zaidi ya pato la Taifa la Tanzania; hivyo ni sehemu ambayo tunaweza kupata wawekezaji wengi katika sekta tofauti,” anasema Kazora.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali katika mitandao zinaonyesha kuwa kipato cha jumla cha jimbo zima la Texas ni Dola trilioni 1.969 za Marekani huku pato la Taifa la Tanzania ni Dola bilioni 56.7 za Marekani.

Kazora ambaye ni mhandisi nchini Marekani alisema tofauti na miaka iliyopita mwaka huu jukwaa hilo litakafanyika kwa siku tatu na litajikita zaidi katika kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini pamoja na kuwatangaza Watanzania mashuhuri ili dunia iweze kuwatambua.

“Kwa miaka iliyopita tumekuwa tukitangaza zaidi utalii wetu Watanzania, lakini sasa tumekuja kwa namna tofauti, utalii tutautangaza kama kawaida lakini sasa tutaitangazia dunia kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania,” alisema Kazora.

Alisema hatua hiyo itasaidia kukuza uwekezaji nchini na kuwanufaisha wananchi ikiwamo kubadilishana ujuzi mbalimbali ambao ni muhimu katika malengo ya sasa ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda.