Diwani wa 18 Chadema ajiunga CCM Kilimanjaro

Deogratias Mushi,aliyekuwa diwani wa Kata ya Kibosho Magharibi kupitia Chadema,akizungumza baada ya kutangaza kukihama chama hicho na kujiunga na CCM

Muktasari:

  • Chadema  kimepata pigo tena baada ya diwani mwingine kujiuzuru udiwani na nyadhifa nyingine alizokuwa nazo ndani ya chama hicho na kujiunga na CCM.

Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Kilimanjaro kimepata pigo baada ya aliyekuwa diwani wa kata ya Kibosho Magharibi halmashauri ya wilaya ya Moshi, Deogratias Mushi kutangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Deogratias Mushi anakuwa diwani wa kwanza kujiuzulu kwa halmashauri ya wilaya ya Moshi na kujiunga CCM na wa 18 katika mkoa wa Kilimanjaro.

Mushi ambaye pia alikuwa Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Moshi ametangaza kujiuzulu nafasi ya udiwani na uenezi leo Aprili 27 na kama ilivyo kwa madiwani wengine ambao wamekihama chama hicho, ameeleza  amefanya hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano za kuwaletea wananchi maendeleo.

"Ninaondoka Chadema kuunga  mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano za kuwaletea Watanzania maendeleo tofauti na wenzangu na kuutokuwa na imani ya kupata maendeleo kwenye halmashauri tukisimamiwa na baraza la madiwani na wabunge wa Chadema," amesema.

Akizungumzia tukio hilo,  Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amesema ni haki yake kujiuzulu na kumtakia mema huko alikokwenda.

"Ni haki yake kuhama chama na ninamtakia mafanikio huko aendako na kile alichokifuata huko akakipate, lakini sisi bado safari inaendelea hadi ifike mwisho," amesema Lema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Kastory Msigala amethibitisha kupokea barua ya kujiuzulu ya diwani huyo na kueleza kuwa kinachofuata kwa sasa ni kuandika barua wizara husika ili taratibu nyingine zifuate.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi alimpongeza Mushi kwa kujiunga na chama hicho na kueleza kuwa watamtumia vyema katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.