Dk Bashiru: CCM haiwezi kuua vyama

Friday January 18 2019

 

By Habel Chidawali na Rachel Chibwete, Mwananchi

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema kitendo cha chama hicho kuunga mkono muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa hakina maana kinataka kuua vyama vingine ili kibaki peke yake.

Amesema sheria ya mfumo wa vyama vingi ilipitishwa kulingana na mahitaji ya wananchi hivyo CCM haina mpango wa kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja kwani hata muasisi wa chama hicho, Mwalimu Julius Nyerere hakupenda kibaki chama kimoja.

Akizungumza jana na wana-CCM wa mkoa wa Dodoma katika mkutano wa chama hicho kupokea maoni ya muswada huo, Dk Bashiru alisema: “CCM ilikubali kupitisha mfumo wa vyama vingi japo kura ya maoni iliyopigwa wananchi wengi hawakuutaka mfumo huo kwa madai ungehatarisha amani ya nchi.”

Alitaja sababu nyingine ni kukithiri kwa rushwa ambayo kama kusingekuwa na chama kingine cha kuinyooshea kidole CCM ikingebweteka.

Naye katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema muswada huo unapingwa na vyama vya upinzani kwa kuwa hawataki yawekwe hadharani madhaifu yao.

Advertisement