Dk Bashiru: Msiihusishe Serikali na matukio ya watu kutekwa, kupotea

Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally akishiriki kujenga ofisi ya Tawi la Songambele Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara leo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema si sahihi kuihusisha Serikali ya Tanzania na matukio ya utekaji wa watu

Simanjiro. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema si sahihi kuihusisha Serikali ya Tanzania na matukio ya utekaji wa watu.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 11, 2019 katika kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro katika siku yake ya kwanza ya ziara yake mkoani Manyara.

Amebainisha kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanatoa taarifa potofu kuhusu watu wanaotekwa na kupotea na kuhusisha matukio hayo na Serikali.

"Ulinzi na usalama ni wajibu wa Serikali, baadhi ya watu kuihusisha (Serikali) na watu wasiojulikana wanaoteka watu hapo watakuwa wanaoichonganisha na watu wake," amesema Bashiru huku akibainisha kuwa mwenye jukumu la kutoa taarifa katika Mkoa ni Mkuu wa Mkoa na kamanda wa polisi wa Mkoa.

“Hao wawili ndio wanapaswa kutoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama ya Mkoa na si viongozi wengine wanaochafua hali ya hewa kwenye mitandao ya kijamii," amesema Bashiru.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Mkoa huo amesema Serikali imepiga hatua kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu, afya, miundombinu ya barabara, umeme na maji.