Dk Bashiru: Wanawake wanaipenda zaidi CCM

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho kinapambwa na kupendwa zaidi na wanawake

Mwanza. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho kinapambwa na kupendwa zaidi na wanawake.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 3, 2019 wakati akizungumza na seneti ya wanafunzi wa vyuo vikuu Mkoa wa Mwanza na kubainisha kuwa chama kinachopendwa na wanawake ni ngumu kukishinda.

“Wanawake wanaongoza kwa kukipamba CCM, chama kikipendwa na wanawake na vijana ndio uhai wake na huwezi kukishinda,” amesema Dk Bashiru

Amesema licha ya uhai wa chama kutegemea wanachama wengi na wapya lakini hawataki wanaoendekeza maslahi yao binafsi bali wanaoweza kujitolea na kukijenga.

Akizungumzia kuhusu chaguzi zijazo ukiwemo wa Serikali za mitaa, Dk Bashiru amesema atakayetumia ukabila, fedha na maslahi binafsi hatavumiliwa.

Amewataka viongozi wa siasa kufuata demokrasia za uchaguzi akidai maadui wa ndani na nje ya nchi wapo na wanaweza kuvuruga amani ya Taifa.

“Atakayetumia uchaguzi kutugawa huyo ni adui wetu, wakati wa uchaguzi ni wakati wa kutafuta viongozi bora na wala sio wa kutafuta machafuko. Wapo ambao wameanza chokochoko, mimi nimewaangalia tu na nimewakalia kimya, wakija hapa Mwanza waone kama adui yenu.”

“Ubepari na ubeberu haujaisha nchini tusipojipanga mikakati hatutaweza kushinda kwenye uchaguzi huo,” amesema Dk Bashiru.