Dk Bashiru ataka wagombea wa CCM wasio na sifa kutopigiwa kura

Muktasari:

Wakati mchakamchaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba, 2019 ukianza katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewataka wanachama wa chama hicho  tawala nchini Tanzania kutowachagua wagombea wa chama hicho wasio na sifa


Mwanga. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amewataka wanachama wa chama hicho kuwanyima kura wagombea wake walevi na wasio na sifa watakaopitishwa katika vikao vya uteuzi kuwania nafasi mbalimbali.

Dk Bashiru aliyepo mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku nne ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 10, 2019 wakati akizungumza na viongozi wa  ngazi mbalimbali wa chama hicho tawala.

“Akiteuliwa mlevi hata kama ni wa CCM mnyimeni kura maana hana sifa huyo. Hakuna sababu ya kuletewa watu wasio na sifa kwa kuwa chama chetu kimesheheni wanachama wenye sifa.”

“Akipitishwa mtu asiye na sifa na mwenye sifa akaachwa wanachama mkataeni ili wanaofanya mchezo washike adabu,” amesema Dk Bashiru.

Amewataka wenye mamlaka ya uteuzi kutojilaumu wakimchagua mgombea asiyefaa, kuwaonya kuacha kuteua watu kwa urafiki, undugu au kuwaacha wengine kwa chuki binafsi.

“Chagueni mgombea mkimlinganisha sifa zake na za Rais John Magufuli. Hicho ndio kielelezo na kila mtakayemteua mjiulize ataweza kufanya kazi na Magufuli. Awe mzalendo kama yeye (rais Magufuli), mwaminifu na mpenda haki anayebeba sifa za chama chetu,” amesema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema wameendelea kujipanga ili kuhakikisha wanapatikana wagombea bora watakaokivusha chama hicho.