Dk Bashiru awaonya polisi kutotumia mabavu kushughulika na wanasiasa

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania cha (CCM) amewataka polisi nchini humo kutokutumia nguvu kushughulikia na migogoro ya kisiasa kutokufanya hivyo.

Kiteto. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk Bashiru Ally amekemea vikali vitendo vya polisi kutumia mabavu bila sababu ya msingi kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya kisiasa.

Bashiru akizungumza jana Ijumaa Julai 12,2019 mji mdogo wa Kibaya wilayani Kiteto mkoani Manyara nchini Tanzania akiwa kwenye ziara, alisema hakuna ulazima wa kutumia mabavu bila sababu maalum.

Alisema mabavu yanapaswa kutumika kama yalivyotumika kumpiga aliyekuwa Rais wa Uganda, Iddi Amin lakini wananchi msivichokonoe na kuvichokoza vyombo vya dola.

"Tukianza kutumia mabavu katika kutatua migogoro yetu ni dalili ya kushindwa kuongoza nchini kwani hakuna sababu ya kuyatumia ili hali wananchi wanatii sheria bila shuruti,” alisema

Alimuagiza mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama havitumii nguvu kubwa bila sababu ya msingi kwani hakuna sababu ya kufanya hivyo.

Alisema nguvu ya ziada inapaswa kuanza kutumika endapo itaonekana kuwa bila mabavu mambo hayawezi kuwa sawa hadi lifanyike jambo hilo.

"Namna tutakavyoona vyombo vyetu vya ulinzi na usalama havitumii mabavu ndivyo tutakavyopima mfumo wetu wa kisiasa, demokrasia na uongozi ulivyo na unavyofanya kazi vizuri," alisema Dk Bashiru.

Hata hivyo, mkuu wa polisi wa wilaya ya Kiteto, Fadhili Luoga alisema kwenye eneo lao hawajawahi kutumia mabavu kwenye ulinzi katika shughuli za kisiasa.

"Chama chochote cha kisiasa kikitaka kufanya mkutano wake wa hadhara kupitia madiwani au mbunge wanatoa taarifa kwetu na tunawapa ulinzi na bila kuwepo na tatizo lolote hatuwezi kutumia nguvu labda pale inapobidi," alisema Luoga.

Katibu wa chama cha NCCR-Mageuzi wilayani Kiteto, Christopher Laizer alipongeza hatua hiyo kwani matukio ya askari polisi nchini Tanzania kuwanyanyasa wapinzani bila sababu ya msingi imekuwa ni kawaida.

"Pamoja na kuwa mimi ni mpinzani ninampongeza sana katibu mkuu wa CCM kwa maneno yake ya kuwaasa polisi kuwa wasitumie mabavu bila sababu ya maana," alisema Laizer.

Katibu mwenezi wa Chama cha Wananchi (CUF), Hassan Mohamed alisema kauli kama hiyo ni ya kujenga demokrasia kwani baadhi ya askari polisi nchini wamekuwa na mtindo wa kuwanyanyasa wapinzani ikiwemo kuwapiga mabomu ya machozi.

Alisema polisi wanapaswa kukaa pembeni na kuwaachia CCM, CUF, Chadema na vyama vingine vipambane jukwaani kwa hoja na siyo kuingilia kati na kunyanyasa wapinzani kama wanavyofanya sasa.