Dk Kihamia aridhishwa na utendaji NEC

Muktasari:

  • Dk Kihamia aeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa Tume ya Uchaguzi, asema wameachana na mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk Athumani Kihamia ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa tume hiyo akieleza kuwa utendaji kazi wa mazoea umepungua.

Amesema katika kipindi alichokaa NEC amegundua kuwa watumishi wengi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa wakati, uaminifu, kutunza siri na kuepuka matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.

Dk Kihamia ameeleza hayo alipokutana na wafanyakazi wa NEC jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya tume. 

Amesema kwa sasa NEC imeimarika vya kutosha kwani alipofika wastani wa utendaji kazi ulikuwa asilimia 52, ikimaanisha kuwa zaidi ya asilimia 48 ya watumishi walikuwa hawawajibiki ipasavyo, lakini sasa uwajibikaji umefikia wastani wa asilimia 65 baada ya kuwekeana malengo.

“Kwa hiyo tulipo sasa tupo juu ila ni lazima tuendelee kuwa kitu kimoja, ingawa katika kuimarika huko wapo wenzetu wachache sana wenye matatizo madogo madogo, hivyo wanatakiwa warekebishwe,” alisisitiza Dk Kihamia.

Amefafanua kuwa kuimarika kwa utendaji kazi ni jambo kubwa kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa kutowajibika ipasavyo kwa watumishi wa umma katika nchi nyingi za Afrika kumesababisha udumavu wa maendeleo ya nchi hizo.

Dk Kihamia amewataka watumishi hao kuendeleza tabia ya uwajibikaji kwa mustakabali wa maendeleo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tanzania kwa ujumla kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuwa chachu ya maendeleo ya nchi.