VIDEO: Dk Mashinji: Hatukushangazwa Lowassa kuondoka

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji 

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji jana Jumatatu alitembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata relini jijini Dar es Salaam na kuzungumza masuala mbalimbali ikiwamo kuondoka kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa aliyerejea CCM


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema hakushangazwa na taarifa ya kuondoka Chadema kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa sababu suala la watu kuwa katika chama na kuondoka ni kawaida.

Dk Mashinji amesema hayo jana Jumatatu Machi 5, 2019 alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata relini jijini Dar es Salaam.

Alisema pengine Lowassa ameona kile alichotarajia hakipo Chadema hivyo ameamua kwenda kukitafuta sehemu nyingine ambayo ni Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katibu mkuu huyo alisema kuondoka kwa Lowassa kumewashangaza kwa kuwa hakumueleza mtu lakini hakiwezi kuathiri chochote. “It was a supprise, ingawa hakiwezi kuathiri chochote, tunamtakia kila la kheri.”

Alipoulizwa iwapo kuondoka kwa waziri mkuu huyo kunaweza kuingilia mikakati ya chama hicho kutokana na kiongozi huyo kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya chama, Dk Mashinji alisema mikakati ya chama hicho iko mezani na kwamba hawahofii chochote.

“Mikakati yetu si ya kigaidi, sisi sio kikundi cha kihalifu, huwezi kuwa na mkakati halafu uwe siri kwa hiyo hakuna ambacho anaweza kupeleka kikatuathiri,” alisema Dk Mashinji.

Alisema Chadema imejenga kinga muda mrefu kwa kukijenga chama kuwa kama taasisi hivyo kuondoka kwake hakutakitingisha na badala yake kitaendelea kuwa imara.

Kuhusu uchaguzi wa mwaka 2020, Dk Mashinji alisema chama chake kimejipanga kushinda kwa kishindo tofauti na watu wanavyofikiri kimekufa.

“Chadema haijafa, kilichobadilika ni jinsi tulivyobadili mfumo wa utendaji kazi, watu walizoea tunajibu kila kitu sasa tumebadili mikakati badala ya uongozi wa juu kuwa ndiyo kila kitu tumezipa nguvu kanda na mikoa,” alisema.

“Tulihakikisha chama kinasambaa katika mikoa, halmashauri na kila kijiji na hilo limefanikiwa leo hii kila kanda tupo tofauti na awali ambako tulikuwa katika baadhi ya maeneo,” alisisitiza Dk Mashinji.

Mashinji ambaye ni daktari wa binadamu pia alimshauri Rais wa Tanzania, John Magufuli kushirikisha watu wote bila kujali itikadi zao kwa kuwa hakuna maendeleo bila demokrasia.

Kufahamu zaidi alichozungumza katika mahojiano hayo, pata nakala ya gazeti la Mwananchi kesho Jumatano Machi 6, 2019