Aliyofanya Edward Lowassa Chadema ndani ya siku 1,312

Edward Lowassa

Muktasari:

Lowassa alisindikizwa Lumumba na rafiki yake wa muda mrefu, Rostam Aziz. Siku Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 26, jijini humo, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema hakuhamia peke yake.


Dar es Salaam. Kujiunga na Chadema kwa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa akitokea CCM baada ya jina lake kukatwa kati ya wagombea urais Julai 2015, kulizua maswali mengi, lakini ujio wake ulikiimarisha chama hicho kikuu cha upinzani katika uchaguzi mkuu mwaka huo.

Hata hivyo, Februari Mosi mwaka huu, Lowassa alitangaza kurejea CCM baada ya kuwa kada wa Chadema kwa siku 1,312. Alipokewa na Rais John Magufuli na viongozi wengine wa ngazi ya juu katika ofisi ndogo za makao makuu chama hicho zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam.

Lowassa alisindikizwa Lumumba na rafiki yake wa muda mrefu, Rostam Aziz.

Siku Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 26, jijini humo, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema hakuhamia peke yake.

“Hatukumkaribisha Lowassa peke yake, tumemkaribisha Lowassa na mamilioni ya Watanzania wengi,” alisema Mbowe huku akiwataka wanachama wao kupokea kile alichokiita heshima ya kuliunganisha Taifa.

“Kama kuna mwana-Chadema asiyeona thamani hiyo kwamba tumepewa heshima ya kulinganisha Taifa, akafikiri mimi kama mwenyekiti ningekataa kupata fursa ya kulinganisha Taifa na kutengeneza mazingira bora ya Taifa letu, huyo tutamwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumjaza busara nikiamini siku za usoni atatuelewa.”

Kuingia kwa Lowassa Chadema kuliwagawa viongozi na wanachama hadi kufikia hatua ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa ambaye alitarajiwa na wengi kuwa angegombea urais kupitia chama hicho, aliachana rasmi na Chadema akipinga hatua ya Lowassa kupokewa.

Kwa upande wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) nako hakukuwa shwari kwani mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliachana na chama hicho akipinga ujio wa Lowassa kwenye kambi hiyo.

Licha ya kupingwa na baadhi ya wapinzani waliomtuhumu kwa kashfa mbalimbali, Lowassa aliweka rekodi ya ushindi tangu kwenye matokeo ya urais hadi kupata wabunge na madiwani wengi ndani ya Ukawa.

Katika uchaguzi huo, Lowassa aligombea urais kupitia Chadema na kupata asilimia 39.97 ya kura zote akimfuatia Rais John Magufuli aliyeshinda kwa kupata kura zaidi ya 8.8 milioni sawa na asilimia 58.46.

Mbali na kuongezeka kwa kura za urais kwa upinzani, Lowassa pia aliwawezesha wapinzani kupata ushindi wa viti 116 vya wabunge katika Bunge la 11 lililoanza Novemba 17, 2015 jijini Dodoma.

Idadi hiyo ya wabunge ndiyo kubwa kuwahi kufikiwa na upinzani tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992, na tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa ushindani wa vyama vingi 1995.

Idadi ya wabunge wa Ukawa iliongezeka baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwateua wabunge wa viti maalumu wa vyama vyenye wabunge wa kuchaguliwa kwa kura za wananchi.

Katika uchaguzi huo uliohusisha majimbo 258 kati ya 262, CCM ilishinda ubunge katika majimbo 188, CUF 35, Chadema 34, NCCR–Mageuzi kiti kimoja. NLD haikupata kiti wakati ACT – Wazalendo ilipata kiti kimoja. Kutokana na majimbo hayo, CCM ilipata viti maalumu 64, Chadema 36 na CUF 10.

Mbali na wabunge, vyama vya Ukawa vilipata nafasi ya kuongoza majiji, halmashauri na miji 26. Miongoni mwa majiji yaliyoshikwa na wapinzani ni pamoja na Dar es Salaam, Mbeya na Arusha huku manispaa zikiwa ni Iringa, Kilimanjaro, Ubungo, Ilala na halmashauri kadhaa.

Wadau wa siasa

Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anasema licha ya kushtushwa na hatua ya Lowassa kurejea CCM, wapinzani hawatakata tamaa.

“Kamwe sikuwa na hata chembe ya mashaka kuwa mzee Lowassa angeweza kutuongoza wanasiasa vijana kwenye upinzani na kutupa uzoefu katika uongozi. Hata hivyo nadhani kuna sababu zenye nguvu zaidi zilizomfanya atumie haki yake ya kikatiba kujiunga tena na CCM,” alisema Zitto.

Alisema wapinzani hawatakata tamaa, bali wataendeleza mapambano ya kuimarisha mfumo wa vyama vingi nchini.

“Kipindi hiki nchi yetu inachopita kinahitaji zaidi vyama imara vya upinzani vyenye umoja kuliko wakati wowote ule katika historia ya nchi yetu. Uchumi unaporomoka na maisha ya watu kuwa magumu zaidi kila kukicha. Tunahitaji zaidi upinzani imara kuliko wakati wowote.”

Kada mkongwe wa CCM, Njelu Kasaka alisema hatua ya Lowassa kurejea ndani ya chama kilichomlea hailengi kupata cheo, bali tulizo la moyo na vilevile kwa chama lengo ni kudhoofisha upinzani.

“Siyo kwamba Lowassa ataongeza nini ndani ya chama, bali ni kudhoofisha tu upinzani. Unajua mbaya wako akiwa na njaa unafaidika. Wala Lowassa haendi CCM kuwa nani, bali anataka utulivu wa maisha ambao anadhani hawezi kuupata akiwa upinzani,” alisema.

Lakini Kasaka alihoji kauli za kejeli alizokuwa akipewa Lowassa na viongozi na makada wa CCM akisema “walisema huyo hana sifa ya kuwa kiongozi, ni mbaya. Hii yote ni kuonyesha kuwa vyama hivi havina misimamo ya kiitikadi, bali vinasukumwa tu na matukio.”