Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia aitangaza Tanzania, akitaja fursa tano kwa wafanyabiashara wa Russia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililofanyika Jijini St. Petersburg nchini Urusi Juni 5, 2026. Kongamano hilo limewakutanisha Wafanyabiashara, Wawekezaji pamoja na Taasisi za kukuza Uwekezaji kutoka Tanzania na Urusi.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ametaja fursa tano ambazo Tanzania inatafuta wawekezaji.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imejipanga kutumia fursa za mabadiliko ya uchumi wa dunia kwa kuvutia wawekezaji wa kimataifa katika sekta za kimkakati zitakazochochea ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo ya viwanda.

Mkuu huyo wa nchi, ameyasema hayo leo, Ijumaa Juni 5, 2026 katika Jukwaa la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026) nchini Russia.

Amesema Afrika ndiyo bara lenye mustakabali mkubwa wa ukuaji wa nguvu kazi duniani, hivyo ni muhimu kuhakikisha ukuaji huo unaleta manufaa kwa wananchi wa Afrika.

“Afrika imekusudiwa kukua na kupiga hatua. Swali kubwa ni itakua kwa masharti gani, kwa ushirikiano na washirika gani, na kwa kutumia mfumo upi wa maendeleo,” amesema Rais Samia.

Katika hotuba yake hiyo, ametaja miradi mitano ambayo Tanzania inatafuta wawekezaji kutoka kwa jumuiya za wafanyabiashara za kimataifa, ikiwemo maendeleo ya miundombinu ya bandari hasa maeneo ya kiuchumi.

“Mradi wa Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo ni mradi namba moja ambao tunakaribisha kampuni za kimataifa kushirikiana nasi,” amesema.

Rais Samia amesema Tanzania inaendelea Bandari ya Mangapwani upande wa Zanzibar na upembuzi yakinifu umekamilika na sasa washirika wanakaribishwa kushirikiana kuwekeza.

Sekta nyingine aliyotaja ni madini, akisema Tanzania ina utajiri wa madini ya uraniam, Nickel, Graphite, Hellium na madini mengine adimu yanayoweza kuleta faida kubwa ya kiuchumi kwa nchi.

“Tunalenga kuondoka kuwa wazalishaji wa malighafi kuwa wazalishaji wa bidhaa iliyokamilika. Tunawakaribisha washirika kuwekeza nasi katika maeneo ya viwanda ambayo yatatoa tafsiri halisi ya faida ya madini,” amesema.

Kwa upande wa sekta ya utalii, amesema Tanzania ni moja ya vituo vinavyojulikana na maarufu kwa utalii ulimwenguni na mwaka jana Hifadhi ya Serengeti ilishinda tuzo ya kuwa hifadhi inayoongoza Afrika.

Amesema Tanzania pia imetunukiwa tuzo ya kuwa moja ya vituo bora vya utalii na ili kuvutia watalii kutoka Russia, imeanzisha safari ya moja kwa moja ya ndege zake kutoka Dar es Salaam hadi Moscow.

“Ndege ya kwanza inatajiwa kuanza safari Julai 2, mwaka huu. Tunalenga kuongeza watalii kutoka Urusi hadi kufikia 500,000 kufikia mwaka 2030 na baadaye milioni moja,” amesema.

Eneo lingine, amesema kama juhudi za mageuzi ya sekta ya kilimo na kuimarisha usalama wa chakula, Tanzania imeweka kipaumbele uzalishaji wa ndani wa mbolea kukidhi mahitaji ya ndani.

Amesema kwa kuwa Russia ni miongoni mwa wasambazaji wakuu wa mbolea duniani, Tanzania inaishawishi kwenda kuanzisha viwanda vya mbolea ili kutoa huduma kwa Taifa na ukanda wa Afrika.

Sekta ya tano ni uzalishaji wa nishati, amesema Tanzania ina kiwango kikubwa cha madini ya Uranium na shabaha yake ni kuyatumia baadhi kuzalisha nishati ya nyuklia ili kufikia mahitaji tarajiwa.

“Katika muktadha huu, Tanzania inaitazama nishati ya nyuklia kama mkakati wake wa muda mrefu wa kuwezesha nishati mchanganyiko ili kuwezesha maendeleo endelevu,” amesema.

Katika kulitimiza hilo, amesema wameandaa mpango wa kuendeleza nishati ya nyuklia na kampuni ya Rosatom ya Urusi imeonyesha utayari na mazungumzo yanaendelea.

“Dunia inakwenda kwa kasi, tunapaswa kwenda upepo unakokwenda. Huu ni muda wa ushirikiano, ukweli na kuaminiana. Zaidi ni muda wa sisi sote kujua fursa zetu,” amesema.

“Tanzania iko wazi kwa ajili ya biashara, Tanzania iko tayari kwa mawazo na ubunifu mpya, Tanzania iko tayari kwa ushirikiano na washirika wa kimataifa. Tunaamini kwamba matokeo ya jukwaa hili yatachangia ipasavyo kukuza ushirikiano katika biashara na uwekezaji,” amesema.


Alichosema Putin

Akizungumza katika jukwaa hilo, Rais wa Russia, Vladimir Putin, amesema dunia inapitia mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanayohamisha nguvu kutoka mfumo wa zamani uliotawaliwa na nchi chache za Magharibi kwenda mfumo wa dunia wenye vituo vingi vya ukuaji wa uchumi.

Amesema nchi nyingi sasa zinatafuta njia mbadala za teknolojia, biashara, fedha na usafirishaji baada ya kushuhudia mifumo ya kimataifa ikitumika kama nyenzo za shinikizo la kisiasa na ushindani usio wa haki.

Putin, ameeleza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Russia na kufungiwa kwa baadhi ya mali zake vimepunguza imani ya mataifa mengi kwa dola ya Marekani na Ulaya.

Akitolea mfano kundi la BRICS, Putin amesema mataifa hayo sasa yanachangia asilimia 40 ya pato la dunia kwa kipimo cha uwezo wa manunuzi (PPP), ikilinganishwa na chini ya asilimia 29 za kundi la G7.

Amesema karibu nusu ya ukuaji wa uchumi wa dunia katika miaka ya karibuni umetokana na nchi za BRICS huku ukuaji wa nchi za G7 ukiwa mdogo zaidi.

Putin pia, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya sarafu za kitaifa katika biashara ya kimataifa, ujenzi wa njia mpya za biashara na mifumo mbadala ya malipo ili kupunguza utegemezi kwa taasisi za kifedha za Magharibi.

Kiongozi huyo ameeleza ushindani wa karne ya sasa utaamuliwa na uwezo wa nchi kujenga teknolojia zake katika akili unde (AI), mifumo inayojiendesha na majukwaa ya kidijitali.

Amesema mataifa yatakayoshindwa kumiliki teknolojia hizo yatajikuta yakitegemea wengine na kupoteza sehemu ya uhuru wao wa kiuchumi na kisiasa.

Putin, amesema nchi yake itaendelea kuimarisha uchumi, kuongeza uwekezaji, kupanua ushirikiano na mataifa rafiki na kulinda uhuru wake wa kiuchumi katika dunia inayobadilika kwa kasi.

Katika hotuba yake hiyo, ameizungumzia nafasi ya Tanzania katika uchumi wa dunia unaobadilika, akisema kuwa moja ya nchi zinazochipukia kama kitovu muhimu cha biashara na ukuaji wa uchumi barani Afrika.

“Tanzania inatekeleza jukumu hilo pia katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema akilinganisha nafasi ya Tanzania katika Afrika Mashariki na ile ya Uzbekistan katika Asia ya Kati.